

1 April 2025, 11:09 am
Taasisi ya jami’iyatul akhlaaqul islam yaadhimisha sikukuu ya idd kwa kutoa msaada kwa wagonjwa hospitali ya Hai.
Na James Gasindi.
Katika kuadhimisha Sikukuu ya Idd, Taasisi ya Jami’iyatul Akhlaaqul Islam imeonesha moyo wa upendo kwa jamii kwa kutoa chakula na vinywaji kwa wagonjwa pamoja na wahudumu wa Hospitali ya Wilaya ya Hai.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Wilaya ya Hai, Sheikh Omary Maamud, alisema lengo la taasisi hiyo ni kushiriki furaha na wale wanaopitia changamoto za kiafya, ili kuwafariji na kuwaombea dua katika kipindi hiki muhimu cha kiimani.
“Sheikh Omary alieleza kuwa taasisi hiyo imekuwa na utaratibu wa kutembelea wagonjwa na watu wenye changamoto mbalimbali kila Jumapili, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kusaidia jamii. Pia, alibainisha kuwa wanashiriki katika kugharamia matibabu kwa wasio na uwezo na kuchangia damu ili kuokoa maisha ya wenye uhitaji.”
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Bomang’ombe, Mheshimiwa Ivod Njau, aliipongeza taasisi hiyo kwa moyo wao wa kujitolea na kutoa wito kwa jumuiya nyingine pamoja na wananchi kuiga mfano huo mzuri wa kusaidia wenye uhitaji.
Naye Fuya Kimbita, mkazi wa Wilaya ya Hai, alisifu hatua hiyo akisema kuwa kutoa sadaka kwa wagonjwa na wenye uhitaji ni kitendo cha thamani kubwa. Akionesha kuunga mkono juhudi hizo, alichangia shilingi laki moja ili kusaidia shughuli za taasisi hiyo.
Mmoja wa wagonjwa waliopokea msaada huo, Marko Lukas, alieleza furaha yake na kushukuru taasisi kwa upendo waliouonesha. “Nimejiona kuwa si peke yangu kwenye changamoto hii. Upendo huu umenipa faraja kubwa, na naomba Mungu aibariki taasisi hii ili iendelee kusaidia wengine wenye mahitaji,” alisema Marko kwa shukrani.
Taasisi ya Jami’iyatul Akhlaaqul Islam imeendelea kuwa kielelezo cha mshikamano wa kijamii, ikijikita katika kusaidia makundi yenye uhitaji kama sehemu ya utekelezaji wa maadili ya kiimani na utu wa kibinadamu.