Prof. Mkenda aeleza maendeleo yaliyofanyika Rombo
22 April 2024, 2:00 pm
Mbunge wa Rombo Profesa Adolf Mkenda afanya mkutano na wajumbe kutoka tarafa ya Mengwe,aeleza miradi kedekede ya maendeleo iliyofanyika na inayoendelea Rombo.
Na Elizabeth Mafie
Mbunge wa Rombo Profesa Adolf Mkenda ambae ndie waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia hapa nchini amesema kuwa maendeleo makubwa ya miradi ya afya,elimu,barabara,pamoja na maji yaliyofanyika Rombo kwa miaka mitatu kwa kupitia fedha walizopewa na Raisi Dkt Samia Suluhu ni kutokana na jitihada na ushirikiano kutoka kwa mkuu wa wilaya hiyo ,viongozi wa chama na serikali pamoja na watendaji wote.
Profesa Mkenda ameyasema hayo katika mkutano wa ndani na wajumbe wa mkutano mkuu wa wilaya CCM kutoka katika tarafa ya Mengwe kwa ajili ya kuelezea maendeleo yaliyofanywa na serikali ya awamu ya sita katika jimbo la Rombo kwa kipindi cha miaka mitatu chini ya Raisi Dkt Samia Suluhu Hassani.
“Na tujue tuu ,ukiona vyaelea ujue vimeundwa ,akikumbia mtu kuna mtu mmoja hata kama anaitwa Adolf Mkenda ,yeye ndio ameleta maendeleo , huyo mtu ni muongo ,haya maedeleo yanaletwa kwa kufanya kazi kwa ushirikiano ,fedha ambazo Raisi wetu ameagiza zishuke kwenye halmashauri,bila kushirikiana kuanzia mbunge ,Dc na watendaji wote na Viongozi wote wa chama na serikali tusingefika hapa tulipofika”Amesema Profesa Mkenda.
Profesa Mkenda amesema kuwa kwa kipindi cha miaka mitatu serikali imetenga mamilioni ya fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika wilaya hiyo ikilinganishwa na miaka kumi iliyopita na kwamba taarafa ya mkuu ilipata kiasi cha shilingi billion 3.8 Mengwe bilioni 3.58,Tarekea billion 2.3, Useri billion 2.49, na Mashati ikipata zaidi ya shilingi million 900.
Pia amewataka viongozi kuanzia ngazi mbalimbali wakiwemo wenyeviti wa vitongoji, vijiji na kata na makatibu wa CCM kata na wenezi kata kuepukana na propaganda ambazo zinakiharibu chama na kuchelewesha maendeleo.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Rombo Raymond Mangwala amewataka wananchi kuendelea kutunza mazingira kwa kupanda miti na kuitunza ili kukabiliana na tabia ya mabadiliko ya nchi na tayari ameshaagiza kila mwanafunzi anatakiwa kupanda miti katika maeneo yao.
Akizungumzia athari za mafuriko zinazoendelea kunyesha hapa nchini amesema kuwa ni vyema wananchi kuchukua taadhari na kwamba kama kuna changamoto kwenye eneo lake ni vyema kutoa taarifa mapema kwa mamlaka husika.
Naye katibu wa CCM wilaya ya Rombo Merry Sulle amewataka viongozi hao kushirikiana ili kushinda katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika siku za hivi karibuni.