Mkenda Super Cup 2024 yazinduliwa rasmi, wachezaji wapewa vifaa vya michezo
31 March 2024, 10:35 am
Mashindano ya Mkenda Super Cup ambayo yalianza rasmi mwaka 2022 katika Jimbo la Rombo yakidhaminiwa na Mbunge wa Jimbo hilo Profesa Adolf Mkenda yazinduliwa rasmi,timu za mpira wa miguu zipatazo 126 kuchuana vikali.
Na Elizabeth Mafie
Mashindano ya Mkenda Super Cup 2024 yamezinduliwa rasmi katika viwanja vya sabasaba Mkuu Rombo na Mkuu wa wilaya hiyo Raymond Mangwala ambapo timu za mpira wa miguu zaidi ya mia moja zinatarajiwa kuchuana.
Akizungumza katika uzinduzi huo mgeni rasmi Raymond Mangwala ambae ndie mkuu wa wilaya ya Rombo amesema kuwa anampongeza mbunge wa jimbo hilo Profesa Adolf Mkenda kwani kwa sasa jimbo la Rombo linaelezea utekelezaji wa ilani inayotekelezwa katika nchi hii na kwamba yeye kama mwenyekiti wa usalama anaona wilaya inakuwa salama vijana wanapokuwa wameitwa pamoja na wanafanya michezo kwani hawafikirii mambo mengine bali wanafikiria michezo.
“Ukija Rombo unayaona matokeo ya utekelezaji wa ilani inayotekelezwa katika nchi hii kwa hiyo tunavyozungumzia Rombo,tunazungumzia liwilaya likubwa,liwilaya lenye mafanikio,lakini hakuna mafanikio yasiyotengenezwa,mkiona vyaelea mjue vimeundwa na mmoja ya mtu aliyeviunda vitu vya wilaya yetu ni Profesa Adolf Mkenda, hongera sana nije kwenye bodi ya ligi niwapongezeni sana bodi ya ligi kazi nzuri na hii mnatusaidia hata sisi kama serikali ,mimi kama mwenyekiti wa usalama ninaona wilaya inakuwa salama vijana wanapokuwa wameitwa pamoja na wanafanya michezo hawafikirii mambo mengine wanafikiria michezo, ni wilaya salama”Amesema Raymond Mangwala.
Awali akielezea nia na madhumuni ya Mkenda Super Cup mratibu wa mashindano hayo Temy Isidory amesema kuwa mashindano hayo yalianza rasmi mwaka 2022 na kwamba yalianza na zaidi ya timu hamsini lakini kwa sasa wana timu zaidi ya mia moja, hivyo mafanikio ni makubwa na mashindano hayo yameleta tija na fursa kwa vijana kwani michezo inawaepusha na vitendo visivyofaa katika jamii pamoja na kuwakutanisha vijana ili wapate kujua kazi mbali mbali zinazofanywa na serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dr Samia Suluhu Hassani.
Nae mbunge wa Rombo Profesa Adolf Mkenda ambae pia ndie waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia hapa nchini na ndie mdhamini wa Mkenda Super Cup amesema kuwa mashindano hayo yatatumika kuwahamasisha vijana kujitokeza kwa wingi kushiriki kikamilifu uchaguzi wa serikali za mitaa pia yatatumika kueleza kazi ambazo serikali imefanya pamoja na kuwakumbusha miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa Rombo ili watakapofanya uchaguzi wafanye uchaguzi sahihi.
Kwa upande wao vijana wanaoshiriki katika mashindano hayo wamemshukuru mbunge wa jimbo hilo Profesa Adolf Mkenda na kwamba mashindano hayo yamekuwa tija na fursa kwao na watayatumia ipasavyo kwani kwa sasa michezo ni ajira huku wakiwasihi vijana wengine kujiunga katika timu za mpira wa miguu ili waweze kunufaika na mashindano hayo.
Katika uzinduzi huo zilichuana vikali timu ya Kelemfua Mokala na Vunjo Fc kutoka Jimbo la Vunjo ambapo timu ya Kelemfua Mokala kutoka Rombo ilimchapa bao 4-0 timu hiyo ya Vunjo FC.