Watakaoharibu uchaguzi serikali za mitaa kukiona
27 March 2024, 7:30 pm
Kutokana na uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu,serikali yatoa onyo.
Na Edwine Lamtey
Serikali imetoa onyo kwa vikundi vya watu,Taasisi ama vyama vya siasa vinavyojipanga kwa ajili ya kuharibu uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.
Waziri wa mambo ya ndani, Mhandisi Hamad Masauni ameyasema hayo wakati anafunga mafunzo ya awali ya polisi kozi namba Moja 2022/2023 katika shule ya polisi Moshi kambi ya Kilele pori wilayani Siha mkoani Kilimanjaro.
Waziri Masauni amelitaka jeshi la polisi kuhakikisha uchaguzi huo unakuwa na amani kwa kujipanga kushirikiana vyema na wananchi ili kupata taarifa za siri kabla uchaguzi kuingia dosari ya aina yoyote.
Katika hatua nyingine waziri Masauni amesema kuwa jeshi la polisi kutekeleza mapendekezo ya tume ya haki jinsi kwa kuhakikisha jeshi haliwi sehemu ya kunyima raia haki zao na unyanyasaji.
Kuhusu uimarishwaji wa jeshi Hilo, waziri Masauni amesema serikali imewekeza miundombinu na vifaa vya kisiasa vikiwamo vya telnolojia ya mawasiliano ili jeshi liweze kuwa la kisasa zaidi
Mapema mkuu wa jeshi la polisi nchini (IGP) Camilius Wambura amesema polisi umejipanga kukabiliana na wale wote wanye nia ya kuvuruga uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu.
Naye mkuu wa shule ya polisi Moshi, Ramadhani Mungi amesema wanafunzi 3701 wamefaulu na kuwa askari huku wanafunzi 193 walishindwa kumaliza mafunzo kutokana na sababu mbalimbali.