Mdau wa maendeleo Hai akabidhi maabara kwa Dc Mkalipa
16 March 2024, 3:41 pm
Katika kuendelea kuunga mkono serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, mdau wa maendeleo wilayani Hai amekabidhi maabara ya kisasa kwa DC Mkalipa.
Na Edwine Lamtey
Serikali wilayani Hai imesema kuwa itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo katika kufanikisha shughuli za kiuchumi na kimaendeleo wilayani humo huku ikizidi kuwaalika wadau mbalimbali ili kushirikiana zaidi.
Kauli hiyo imetolewa na Amir Mkalipa Mkuu wa Wilaya ya Hai wakati akikabidhiwa maabara mpya ya kisasa kwa masomo ya sayansi iliyojengwa na Mega Bevarage Limited chini ya mkurugenzi wake Fransis Kimaro, maabara ambayo imejengwa katika shule ya sekondari Marire.
Mkalipa amesema kitendo cha mwananchi mzawa wa eneo hilo kukumbuka shule aliyosoma na kuifadhili jengo la maabara kinafaa kuigwa na jamii ya watanzania kwa manufaa ya vizazi vya sasa na baadaye.
“Sisi kama wilaya tunampongeza mkurugenzi wa Mega Bevarage Ltd hakika kiasi hiki cha fedha angeweza kufanyia biashara yake nyingine ila busara yake ameona awekeze katika kusaidia elimu ya watoto wetu, na naambiwa na yeye alisoma hapa; hongereni sana wazazi na jamii yq hapa kwa msingi huu mzuri kwa vijana wetu”. Alisema Mkalipa.
Akimwakilisha mkurugenzi wa Mega Bevarage Ltd Bi. Neema Uisso amesema kuwa wataendelea kushirikiana na serikali katika kuhakikisha kuwa wanaileta jamii maendeleo.
Awali akisoma risala mkuu wa shule ya sekondari Marire Mwalimu Namkanda Kagonji amesema kuwa ujenzi wa maabara hiyo hadi kukamilika kwake umegharimu kiasi cha Shilingi milioni 81.6 ambapo kukamilika kwa ujenzi huo kunaifanya shule hiyo kwa sasa kufikisha idadi ya maabara tatu zinazoweza kuwasaidia wanafunzi kufanya mazoezi kwa vitendo.
Katika hatua nyingine akitoa salamu za Mbunge wa jimbo la Hai Saashisha Mafuwe, mkuu wa wilaya ya Hai Amir Mkalipa ameaasa wazazi kutambua kuwa jukumu la kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula shuleni ni lao badala ya kuiachia serikali pekee huku akisema serikali inaendelea na ujenzi wa miundombinu mbalimbali.