Baraza la madiwani wilaya ya Siha lampongeza mkurugenzi wa halmashauri hiyo
22 February 2024, 12:37 pm
Kutokana na jitihada za Mkurugenzi mtendaji pamoja na watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya siha za ukosanyaji wa mapato,baraza la madiwani wa halmashauri hiyo latoa pongezi.
Na Elizabeth Mafie
Baraza la madiwani wilaya ya Siha mkoa wa Kilimanjaro limempongeza mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri hiyo Dkt Haji Mnasi pamoja na watumishi kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali.
Pongezi hizo zimetolewa na mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Dunkan Urassa kwa niaba ya madiwani wa Halmashauri hiyo wakati akiwasilisha taarifa yake ya katika mkutano wa kawaida wa baraza la madiwani ulioketi katika ukumbi wa mkutano wa halmashauri hiyo katika kipindi Cha robo ya pili ya mwaka wa fedha 2023/2024.
Hata hivyo Dankani amesisitiza kuongezwa kwa juhudi kubwa zaidi katika ukusanyaji wa mapato ya halmashauri iili yasaidie katika kuboresha utoaji wa huduma mbalimbali kwa wananchi na kusema kwamba ni vyema fedha hizo zikatumika kulingana na bajeti inavyoelekeza.
Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo Dkt Haji Mnasi ameelezea mbinu walizofanya katika kuongeza mapato pamoja na mikakati waliyojiwekea kama halmashauri katika kuendelea kuboresha vyanzo vya mapato.
Amesema kuwa mapato ya ndani wamekusanya kwa asilimia 84 na matarajio yao ni kuweza kufikisha asilimia mia moja na kwamba anawashukuru kwa ushirikiano madiwani wote wa halmashauri hiyo na watendaji kwa ujumla na wote walioshiriki kwa namna yoyote.
Nae mkuu wa wilaya hiyo Dtk Christopher TImbuka amewakumbusha wananchi kushiriki katika mbio za mwenge wa Uhuru unaotarajiwa kuwashwa mkoani Kilimanjaro Aprili 2 2024 katika viwanja vya ushirika Moshi mjini hivyo ni vyema viongozi kuhamasisha wananchi ili waweze kushiriki kwa wingi hata utakapo wasili katika wilaya ya Siha.
Hata hivyo baraza Hilo limeketi kwa lengo la kupitia taarifa mbalimbali za utekelezaji wa halmashauri ikiwemo utekelezaji wa miradi ya maendeleo, taarifa za mapato na matumizi, na taarifa ya utekelezaji kutoka kata zote 17 za wilaya hiyo.