Triple A FM

Unamtafuta kamanda wa polisi Arusha? Anakuja

8 October 2026, 11:18 am

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, SACP Justine Masejo akizungumza na wanafunzi wa shule ya Mringa

Na Joel Headman

Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limezindua rasmi kampeni ya “Ongea na Kamanda wa Polisi” katika Shule ya Sekondari Mringa iliyopo wilaya ya Arumeru mkoani hapa, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kutatua kero za kiusalama na kuimarisha ushirikiano kati ya Polisi na jamii

Akizungumza wakati akizindua kampeni hiyo Oktoba 07, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, SACP Justine Masejo amesema kampeni hiyo itaendelea katika maeneo mbalimbali ya Mkoa kwa lengo la kuwapa wananchi nafasi ya kuwasilisha taarifa, changamoto na kero za kiusalama moja kwa moja kwa Jeshi la Polisi

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, SACP Justine Masejo

Amesema ushirikiano huo unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa taarifa za uhalifu na viashiria vyake, huku ukiwawezesha wananchi kufahamu majukumu ya Polisi na namna sahihi ya kufikisha taarifa au kero zao katika maeneo yanayohusika ili hatua zichukuliwe kwa wakati

Kwa upande wake Bi. Neema Weston, mwanafunzi wa Kidato cha Sita katika Shule hiyo, amesema wamefurahishwa na ujio wa Polisi shuleni hapo kutokana na kupata elimu kuhusu namna ya kujiepusha na vitendo vya uhalifu na matumizi ya dawa za kulevya, akisema elimu hiyo itawasaidia vijana kujenga maisha yenye mwelekeo mzuri

Mwanafunzi wa Mringa akitoa maoni