Triple A FM

Mvua za juu ya wastani kunyesha ndani ya kipindi cha siku tano zijazo-TMA

7 December 2023, 2:20 pm

Mkurugenzi wa Miundombinu na Huduma za ufundi wa ,Mamlaka ya hali ya hewa nchini Dokta Paskali Wanyiha,akielekeza jambo.Picha na Anthony Masai.

Licha ya maeneo mengi ya nchi kuendelea kupata mvua za kiwango cha juu ya wastani na kusababisha mafuriko katika baadhi ya maeneo,Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini TMA imesema mvua hizo zitaendelea kunyesha ndani ya siku tano zijazo.

Na.Anthony Masai

Wakati baadhi ya wilaya za mikoa ya Tanzania bara zikiripotiwa taarifa za maafa yatokanayo na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema kuwa ndani ya kipindi cha siku tano zijazo mvua kubwa zitaendelea kunyesha katika maeneo hayo.

Mkurugenzi wa Miundombinu na Huduma za ufundi wa Mamlaka ya hali ya hewa nchini Dkt. Paskali Wanyiha akihojiwa na Triple A Fm jijini Arusha amesema utabiri wa muda mrefu unaonesha kwamba mvua zitaendelea hadi miezi ya mwanzoni mwakani lakini kuna utabiri muhimu ambao hutolewa kwa kipindi cha siku tano hadi wiki mbili.

Dkt. Wanyiha amesema katika kipindi cha siku tano hadi wiki mbili zijazo, maeneo mengi ya nchi yataendelea kupata mvua za juu ya wastani ikiwemo maeneo ambayo yameripotiwa kutokea mafuriko ikiwemo Kilosa.

Sauti ya Mkurugenzi wa Miundombinu na Huduma za ufundi wa TMA Dkt. Paskali Wanyiha

Aidha ametoa wito kwa wananchi kuendelea kufuatilia utabiri wa hali ya hewa unaotolewa na mamlaka ya hali ya hewa nchini, ikiwa ni pamoja na kufuata ushauri unaotolewa ili kuepusha madhara zaidi hasa katika maeneo ambayo yanapata mvua nyingi.

Akizungumzia utabiri wa TMA kwa wilaya za Mkoa wa Manyara ikiwemo maeneo yaliyopata maafa ya Kateshi,Mkurugenzi huyo amesema timu ya wataalamu kutoka katika ofisi za Mamlaka hiyo bado ipo katika maeneo hayo na itatoa taarifa,itakapokuwa tayari.