Triple A FM

Hivi ndivyo ajali ilivyoua 15 Arusha

24 February 2024, 10:26 pm

Kamanda wa polisi mkoa wa Arusha SACP Justine Masejo akizungumza eneo la Ngaramtoni kulipotokea ajali

Na Joel Headman.

Watu 15 wamefariki dunia papo hapo mkoani Arusha katika ajali ya barabarani iliyohusisha magari matatu.

Akiwa katika eneo la Kibaoni Ngaramtoni ilikotokea ajali hiyo, Kamanda wa polisi mkoa wa Arusha SACP Justine Masejo amesema ajali hiyo imetokea leo Feb 25 majira ya saa 11 jioni baada ya lori lililokuwa likitokea Namanga kuelekea Arusha kuyagonga magari matatu.

Shughuli za unasuaji wa magari yaliyohusika kwenye ajali zikiendelea

Akizungumza bila kutaja jina la dereva aliyekuwa akiendesha lori hilo, Kamanda Masejo ameeleza kuwa taarifa za awali zinaonyesha lilipoteza uelekeo hali iliyopelekea kuyagonga magari hayo.

Kwa mujibu wa kamanda Masejo majeruhi wa ajali hiyo wapo katika hali mbaya na wanaendelea na matibabu. Hata hivyo amewaomba wananchi ambao ndugu zao walikuwa wakisafiri kupitia barabara hiyo kufika katika hospitali ya mkoa wa Arusha Mount Meru kwa ajili ya utambuzi wa marehemu pamoja na majeruhi ambao wanatibiwa hapo

Sauti ya kamanda wa polisi mkoa wa Arusha SACP Justine Masejo