Triple A FM

Serikali inapoteza mapato kwa wanahabari kutokuwa na mikataba – JOWUTA

19 March 2024, 1:23 pm

Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi Waandishi wa Habari nchini (JOWUTA), Mussa Juma. Picha na Anthony Masai.

“Asilimia 80 ya waandishi wa habari nchini hawana mikataba ya ajira”

Na Anthony Masai

Chama cha wafanyakazi katika vyombo vya habari nchini (JOWUTA) kimesema wakati Serikali ikiendelea na mchakato wa kuirasmisha sekta ya habari nchini,inaendelea kupoteza mapato mengi ambayo yangetokana na kodi za mishahara ya wafanyakazi katika vyombo vya habari ambao hawana mikataba ya ajira.

Akizungumza katika kikao cha tathmini ya Sekta ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Wadau wa Sekta hiyo kilicho fanyika jijini Arusha, Mwenyekiti wa JOWUTA Mussa Juma amesema asilimia 80 ya waandishi wa habari nchini hawana mikataba ya ajira.

Juma amesema iwapo serikali itatatua changamoto hiyo ni wazi kuwa serikali itaongeza mapato kutokana na michango ya kodi na mapato kutoka kwa waandishi hao takribani elfu kumi waliopo nchini.

Amesema mbali na kutochangia pato la taifa lakini changamoto ya kukosekana kwa mikataba imesababisha waandishi kukabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo za kiuchumi hasa pale wanapougua au kuuguliwa.

Sauti ya Mussa Juma

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri nchini Deodatus Balile ameiomba serikali kutoa mtaji katika vyombo vya habari ili kutimiza malengo ya vyombo hivyo pamoja na kukuza uchumi wa nchi.

Akifungua mkutano huo ambao ni wa majadiliano ;Waziri wa Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema Ushirikiano kati ya Wizara hiyo na Sekta zingine umeimarishwa tofauti na ilivyokuwa huko nyuma ambapo kwa sasa Serikali kupitia vyombo vyake kama TCRA wamekuwa rafiki wa wadau.