Triple A FM
Triple A FM
12 September 2026, 11:08 am

“Zoezi hili kwa uzoefu wangu tulifanye kwa ushirikishwaji…..Baada ya kikao changu mkutane na viongozi wa Wamachinga katika maeneo yenu”
Na Joel Headman
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Amos Makalla amewaagiza wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri na maofisa tarafa kusimamia kwa nguvu kampeni ya usafi wa mazingira ili kuendana na hadhi ya Arusha kama kitovu cha utalii na kuitwa Geneva ya Afrika.
Makalla ametoa agizo hilo Septemba 11, 2026, katika kikao na watendaji kutoka Wilaya za Arusha na Arumeru, akiwataka kuhakikisha mazingira yanakua safi hasa katika maeneo maalum ya kimkakati yanayotambulisha mkoa.
Akibainisha miongoni mwa njia zitakazotumika ameeleza kuwa ni Pamoja na kuondolewa kwa wafanyabiashara wanaofanya biashara barabarani na mbele ya maeneo ya biashara rasmi
Ameelekeza kampeni hiyo kuanzia kwenye maeneo yanayoonekana zaidi, yakiwemo pembezoni mwa barabara zinazoelekea Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro, Uwanja wa Ndege Arusha, mpaka wa Namanga na katikati ya Jiji.
Makalla pia amewaagiza watendaji kutumia vyombo vya habari kutoa elimu ya usafi kuanzia ngazi ya kaya, mtaa, kata, wilaya hadi mkoa