Triple A FM
Triple A FM
14 September 2026, 1:45 pm

“Mi mwenyewe binasfi kweli wanasemaga mwanaume unatakiwa uwe Jasiri,,,mimi kwa tukio nililo liona huo ujasiri nilikosa….kwa sababu mimi ni kitu ambacho nilishaambulia kuliona kwenye muvi (filamu) tu, ila…..”
Na Joel Headman
Ndugu wa kijana Hamis Idd Masimba wameliomba jeshi la polisi mkoa wa Arusha kuwasaidia kupata ukweli juu ya kifo chenye utata cha ndugu yao aliyekuwa dereva wa bodaboda jijini Arusha
Akiongea na waandishi wa Habari kaka wa marehemu Hamis ameeleza kuwa licha ya juhudi zilizofanikisha kupatikana kwa mwili wa mdogo wao, bado wana kiu ya kuhitaji ukweli wa chanzo cha kifo na wahusika
Ameeleza kuwa mchakato wa kumtafuta ndugu yao ulianza baada ya kutoweka kwake kwa siku kadhaa bila kuonekana
Kupitia taarifa ya jeshi la polisi mkoa wa Arusha iliyotolewa kwa Triple A fm jana, tayari uchunguzi wa tukio hilo na mengine umeanza na unaendelea
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa na kamanda wa polisi mkoa wa Arusha SACP Justine masejo, tayari watu kadhaa wanashikiliwa wakihusishwa na mtandao wa kihalifu unaojumuisha mauaji, Unyang’anyi wa kutumia silaha na wizi wa pikipiki
Miongoni mwa matukio hayo ni tukio la mauaji ya Anold Osward (28) mkazi Orolesho, kata ya Olasiti Jijini Arusha yaliyotokea Juni 19, 2026 katika Mtaa wa Olteves, kata ya Olmot Jijini Arusha ambapo baada ya mahojiano ya kina watuhumiwa hao walikiri kuhusika katika tukio hilo na matukio mengine katika wilaya ya Arumeru Kamanda Masejo amebainisha kuwa uchunguzi wa wa tukio la mauaji ya Hamis Idd Masimba (22) dereva wa bodaboda na mkazi wa Olasiti, ambaye alipotea na baadaye mwili wake ulipatikana Septemba 12, 2026 ndani ya nyumba ambayo haijakamilika, iliyopo maeneo ya Stendi Mpya, Mtaa wa Bondeni City jijini Arusha
Kamanda Masejo amewasihi waendesha bodaboda na wamiliki wa pikipiki kuwa makini wanapobeba abiria au kukodisha pikipiki zao kwa ajili ya safari, hususani nyakati za usiku, kuhakikisha wanatoa taarifa mapema pindi wanapobaini mwenendo wowote wa kutia shaka.