Pambazuko FM Radio

Six rivers Africa watumia Tsh. Mil 45.5 kuwezesha Vikundi 13 vilivyopakana na hifadhi ya Taifa ya Nyerere-Ifakara

21 December 2024, 9:54 am

Na Katalina Liombechi

Shirika la Six Rivers Africa limehitimisha zoezi la kukabidhi Miradi ya kujikwamua kiuchumi kwa awamu hii kwa Vikundi 13,Kutoka vijiji vilivyopakana na Hifadhi ya Taifa ya Nyerere ikiwa ni miradi yenye thamani ya Tsh.Mil 45 na laki tano.

Kwa Mujibu wa Irene Masonda Afisa Miradi kutoka shirika hilo amesema lengo ni kuziinua kiuchumi jamii zilizopakana na hifadhi ya Taifa ya Nyerere ili jamii hizo ziache kutegemea Rasilimali kutoka hifadhini kujipatia kipato.

Picha ya Irene Masonda Afisa Miradi Six rivers Africa(Picha na Katalina Liombechi)
Sauti ya Irene Masonda Afisa Miradi Six rivers Africa

Mkuu wa Idara maendeleo ya Jamii Halmshauri ya Mji wa Ifakara Bi.Florence Mwambene amevitaka vikundi vilivyofadhiliwa miradi na Shirika la Six rivers Africa kujiendesha kwa faida ili kupata uendelevu.

Akizungumza akiwa kijiji cha Miwangani Kata ya Sanje amesema idara yake itahakikisha inafuatilia miradi hiyo kwa ukaribu ili kuona namna inavyofanya kazi na kwamba Serikali ijivunie mafanikio kutokana na Matokeo chanya kama ambavyo Six rivers Africa inavyotarajia.

Sauti ya Mkuu wa Idara maendeleo ya Jamii Halmshauri ya Mji wa Ifakara Bi.Florence Mwambene
Picha ya Bi.Florence Mwambene Mkuu wa Idara maendeleo ya Jamii Halmshauri ya Mji wa Ifakara(Picha na Katalina Liombechi)

Wakizungumza Mara baada ya Kupokea Miradi hiyo baadhi ya Wanufaika wameahidi kuifanyia kazi na kuacha shughuli za kuingia hifadhini kuvua samaki,kulima kukata mkaa na badala yake watakuwa mabalozi wa kutoa elimu juu ya umuhimu wa kuhifadhi rasilimali hizo muhimu kwa matumizi ya baadaye huku Mwenyekiti wa Kijiji cha Sagamaganga Ismail Adam Abdulkadir akisisitiza hakuna pesa inayowekezwa pasi ya kuwa na kazi bali ni dhamira ya serikali na wadau kuona umuhimu wa kuinua uchumi wa watu.

Sauti za Wanufaika Miradi iliyowezeshwa na Six rivers Africa
Picha ya Baadhi ya Wanufaika wa Mradi wa kutengeneza Sabuni Kata ya Kiberege(Picha na Katalina Liombechi)

Vikundi vilivyonufaika ni pamoja na Upendo kutoka katindiuka,Nguvu Moja kutoka Lungongole,Tumaini na Jikwamue kutoka Nyamwezi,Utulivu na Mishemishe kutoka Nkasu,Mshikamano na Upendo kutoka Bwani huku Katika Kata ya Mwaya ni vikundi vya Mazingira Foundation  na Tunza mazingira kutoka kijiji cha Mikoleko na Kikundi kingine kutoka Mhelule.

Aidha Vikundi vingine ni Mwanzo bora na Tujiendeleze kutoka kijiji cha Miwangani kata ya sanje pamoja na Kikundi cha Faraja kutoka Sagamaganga Kata ya Signal ambapo vimenufaika kwa Miradi ya Ufugaji nguruwe,Biashara ya kuongeza Mnyororo wa thamani mazao ya Nafaka,kuuza maziwa ya Ng’ombe na Utengenezaji wa Sabuni na kwamba kila mradi unagarimu kiasi cha Tsh.Mil 3.5.

Picha ya pamoja Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya jamii Ifakara Bi.Florence Mwambene na wanakikundi cha Jiendeleze Kijiji cha miwangani Sanje