Pambazuko FM Radio

Six Rivers Africa wakabidhi miche 16,090 kuunga mkono serikali

21 November 2024, 2:13 pm

Na Katalina Liombechi

Six rivers Africa Wameenda na kauli mbiu ya Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutuletea miche ya Kimkakati ili kuhakikisha kwamba wananchi wanafaidika na kujipatia kipato.

Shirika lisilokuwa la Kiserikali linalojihusisha na Uhifadhi wa Wanyamapori na kukuza Uchumi kwa Jamii zinazopakana na hifadhi Katika Wilaya ya Kilombero  Six rivers Africa wamekabidhi Miche zaidi ya 16,090 kwa Wakulima Vijiji 12 vinavyopakana na Hifadhi za Taifa za Nyerere lengo likiwa ni kukuza uchumi wa Watu na kuendelea kutunza mazingira.

Akipokea Miche hiyo ya Mazao ya Kimkakati Mkuu wa Wilaya amelishukuru Shirika hilo kwa kuendelea kuiunga Mkono Serikali kuwapatia wananchi Miche ambayo  inakwenda kukuza uchumi wao na kufanya Uendelevu wa Mazingira.

Ametumia hafla hiyo kuwataka wakulima kuhakikisha miche hiyo inakuwa huku akiwaagiza Afisa Kilimo,Wahifadhi,Afisa maendeleo ya Jamii na watendaji kuisimamia na kufanya ufuatiliaji kuhakikisha miche inaleta manufaa ambayo Six rivers Africa na Serikali inayatarajia.

Pamoja na mambo mengine Mkuu wa Wilaya amesema Mradi Mkubwa wa Kimkakati wa Bwawa la Mwalimu Nyerere unaotekelezwa na Serikali ya Tanzania uendelevu wake unategemea Asilimia 65 ya Maji yanayotoka katika Mto Kilombero hivyo inahitajika Jitihada za pamoja kutunza rasilimali zote muhimu ambazo pia ni tunu kwa Taifa.

Picha ya Pamoja Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Wakili Dunstan Kyobya akiwa na wadau wa Mazingira baada ya kukabidhiwa miche(Picha na Katalina Liombechi)
Sauti ya Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Wakili Dunstan Kyobya

Afisa Mradi wa Six rivers Africa Irene Masonda ameelezea lengo la kukabidhi miche hiyo ambapo amesema wakulima wanaonufaika ni 235 na kusema kuwa wao wanaamini uchumi wa Watu ukiimarika itafanya jamii kuwa tayari na kuona umuhimu wa dhana ya kuishi pamoja na Wanyamapori kwa uendelevu wa Shughuli za Uhifadhi huku akitaja vijiji vinavyonufaika na Mradi huo.

Sauti ya Irene Masonda Afisa Mradi Six rivers Africa

Picha ya Irene Masonda Afisa Mradi Six rivers Africa(Picha na Katalina Liombechi)

Wadau wa Uhifadhi,kilimo na Maendeleo ya jamii wamesema Miche ya Mazao hayo yatasaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha maisha ya watu na kupunguza Migogoro na wahifadhi hali itakayowafanya kutokutegemea Rasilimali za asili kutoka katika Maeneo yaliyohifadhiwa.

Picha ya Wadau wa uhifadhi(Picha na Katalina Liombechi)
Sauti za Wadau wa uhifadhi

Miche hiyo ambayo imekabidhiwa Novemba 21,2024 ni pamoja na Kokoa,Chikichi,korosho na karafuu ambapo wakulima 235 kutoka vijiji 12 vilivyopakana na hifadhi ya Taifa ya Nyerere ikiwa ni pamoja na Katindiuka,mbasa,Lungongole,Sagamaganga,Signal,Nkasu,Nyamwezi,Bwawani,Msalise,Mikoleko,Mhelule na Miwangani.