Highlands FM

Wazazi wakumbushwa kuwa karibu na watoto Wakati wa likizo

3 July 2025, 11:31

Mkurugenzi wa Shule ya Holyland Pre and Primary School Lawena Nsonda.Picha Samwel Mpogole

Ni wito unaowataka wazazi na walezi kuwa makini dhidi ya vitendo vya ukatili na udhalilishaji kwa watoto.

Na Samwel Mpogole

Wazazi na walezi wametakiwa kuwa na mshikamano wa karibu na watoto wao hususan katika kipindi cha likizo, ili kuwakinga na vishawishi vya maisha ya mitaani ambavyo vinaweza kuathiri mustakabali wa maisha yao ya baadaye.

Wito huo umetolewa na Afisa Ustawi wa Jamii wa Mkoa wa Mbeya, Bi. Aika Temu, alipokuwa akizungumza na Highlands FM radio ofisini kwake, ambapo ameeleza kuwa likizo ni kipindi nyeti kinachohitaji usimamizi makini wa wazazi ili kuwalinda watoto dhidi ya mwelekeo usiofaa.

“Tunaendelea kushuhudia baadhi ya watoto wakitoroka nyumbani na kujiingiza mitaani kwa sababu ya kukosa uangalizi wa karibu kutoka kwa wazazi wao. Wazazi wanapaswa kutumia muda huu wa likizo kujenga mawasiliano ya karibu na watoto wao,” 

Sauti Aika Temu

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa shule ya Holyland Pre and Primary School iliyopo Makongoro, Bw. Lawena Nsonda maarufu kwa jina la Baba Mzazi amesisitiza umuhimu wa kipindi cha likizo kutumiwa kama daraja la kuimarisha mahusiano ya kifamilia.

“Wakati wa likizo ndiyo fursa sahihi kwa mzazi kuwa karibu na mtoto wake. Kutowajibika katika kipindi hiki kunaweza kusababisha athari kubwa za kisaikolojia na kijamii kwa mtoto, ikiwemo kujiingiza katika makundi mabaya,” 

Sauti Lawena Nsonda

Kauli hizo zimekuja wakati ambapo baadhi ya jamii zimeendelea kushuhudia ongezeko la watoto wa mitaani, hasa katika mikoa ya nyanda za juu kusini, hali inayochangiwa na uzembe wa baadhi ya wazazi kushindwa kutimiza wajibu wao ipasavyo.