Highlands FM
Highlands FM
24 June 2025, 11:30

Wazazi watakiwa kuwa ngao ya kwanza ya ulinzi kwa watoto kipindi cha likizo.
Na Samwel Mpogole
Wazazi na walezi wametakiwa kuwa karibu na watoto wao hasa katika kipindi hiki ambacho shule zimefungwa, ili kuwalinda dhidi ya vitendo vya ukatili vinavyoweza kuwakumba wakiwa majumbani au mitaani.
Wito huo umetolewa na Afisa kutoka Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, kupitia Kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto, ASP Loveness Mtemi, alipokuwa akizungumza na Highlands Fm. Amesema ni wajibu wa kila mzazi kuhakikisha anajua watoto wake wapo wapi, wanafanya nini, na wanahusiana na nani katika kipindi hiki cha likizo.
Kwa upande wake, Mrakibu Msaidizi wa Polisi Fridah Thadei kutoka ofisi hiyo hiyo, ameitaka jamii kushirikiana kikamilifu na jeshi la polisi kwa kutoa ushahidi mahakamani pindi watuhumiwa wa ukatili wanapokamatwa, akisisitiza kuwa tabia ya baadhi ya wazazi kutaka kumaliza kesi za ukatili kimya kimya ni hatari kwa ustawi wa watoto.
Nao baadhi ya wazazi na wananchi mkoani Mbeya wameeleza mitazamo yao juu ya wito huo, wakisisitiza umuhimu wa malezi ya karibu na kuunga mkono juhudi za polisi katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia na watoto.