Boma Hai FM

Zaidi ya kaya 500 zakumbwa na mafuriko kata ya Kia wilayani Hai

24 March 2026, 12:12

Pichani ni Mbunge wa jimbo la Hai Saashisha Mafuwe(aliyevaa miwani)akiwa na baadhi ya wananchi wa kata ya Kia mara baada ya kukumbwa na mafuriko(picha na Mwandishi wetu)

Kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha nchini, zaidi ya kaya 500 katika kata ya Kia wilayani Hai mkoani Kilimanjaro zimekumbwa na mafuriko yaliyosababisha baadhi ya wananchi kuyahama makazi yao na kuathiri shughuli za kijamii na kiuchumi, huku wakazi wakieleza kuwa mabadiliko ya miundombinu ya makalavati katika barabara ya Moshi -Arusha yamechangia kuongezeka kwa mtiririko wa maji kuelekea maeneo ya chini, hali iliyosababisha wanafunzi kushindwa kwenda shule na biashara ndogo ndogo kusimama, wakati mamlaka husika zikiahidi kuchukua hatua za kudhibiti tatizo hilo.

Na Elizabeth Mafie

Hai – Kilimanjaro

 Kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha hapa nchini, wananchi wa kata ya kia wilayani Hai mkoani Kilimanjaro wamekumbwa na athari za mafuriko yaliyosababisha zaidi ya kaya 500 kuathirika.

Taarifa kutoka eneo hilo zinaeleza kuwa baadhi ya wakazi wamelazimika kuyahama makazi yao baada ya maji kujaa katika nyumba zao, hali inayosababisha usumbufu mkubwa wa maisha na kuhatarisha usalama wao.

Wakizungumza kuhusu hali hiyo Machi 23,2026 wananchi wa kata  ya Kia  wameeleza kuwa changamoto kubwa inayochangia mafuriko hayo ni ukarabati unaoendelea wa makalavati katika barabara kuu ya Moshi –Arusha ambapo umebadilisha mwelekeo wa maji na kusababisha maji mengi kutoka wilaya za Siha  na Arumeru  kuelekezwa katika maeneo ya chini,hasa  kata ya Kia .

Sauti ya Mwananchi kata ya Kia akielezea changamoto walizokutana nazo baada ya mafuriko hayo.

Akizungumza baada ya kutembelea maeneo yaliyoathirika, Mbunge wa jimbo la Hai Saashisha Mafuwe amesema mafuriko hayo yameathiri kwa kiasi kikubwa shughuli za kijamii na kiuchumi, ikiwemo wanafunzi kushindwa kufika mashuleni pamoja na kusimama kwa shughuli ndogo ndogo za kiuchumi.

Sauti ya mbunge wa jimbo la Hai Saashisha Mafuwe.

Ameeleza kuwa maboresho ya miundombinu ya makalavati katika eneo la mjooroni yamechangia mabadiliko ya mtiririko wa maji, hali iliyosababisha maji kuelekezwa kwa wingi katika maeneo ya chini na kuongeza ukubwa wa tatizo hilo.

Kwa upande wake  Meneja Wakala  wa Barabara  (TANROADS) mkoa wa Kilimanjaro  Mhandisi Motta Kyando amesema zipo hatua mbalimbali watakazochukua ili kukabiliana na changamoto hiyo pamoja na kutoa tahadhari kwa wananchi wanaoishi katika maeneo hatarishi.

Sauti ya Meneja TANDOADS mkoa wa Kilimanjaro Mhandisi Motta Kyando

Wakati huo huo, vijiji vya Mtakuja na Tindigani  vinaendelea kuathirika na mafuriko yanayotokana na bwawa la Kidawashi lililopo wilaya ya Simanjiro, huku kijiji cha Sanya Station nacho kikikumbwa na maji yanayotoka wilaya za  Siha  na Arumeru.

Pichani ni Mbunge wa Jimbo la Hai Saashisha Mafuwe pamoja na Diwani wa Kata ya Kia Tehera Mollel wakiwa kwenye mtumbwi(picha na Mwandishi Wetu)

Katika hatua nyingine Saashisha amesema tayari amewasiliana na mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro kuhusu tatizo hilo, ambapo ameahidi kuunda tume ndogo ya uchunguzi itakayofuatilia chanzo cha mafuriko hayo na kupendekeza suluhisho la kudumu.

Pichani ni Meneja TANROADS mkoa wa Kilimanjaro Mhandisi Motta Kyando akielekeza jambo(picha na Mwandishi wetu)