Boma Hai FM
Boma Hai FM
13 March 2026, 2:45 pm

Kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali hapa nchini wito umetolewa kwa watumiaji wa barabara pamoja na madereva kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa vyombo vyao vya moto ili kuepusha ajali.
Na Oliva Joel
Hai -Kilimanjaro
Katika kipindi hiki cha mvua, madereva na watumiaji wengine wa barabara wametakiwa kukagua vyombo vyao vya moto mara kwa mara ili kuepuka ajali.
Hayo yameelezwa leo Machi 13, 2026 na Sajenti Ramadhani Juma kutoka kituo cha Polisi Bomang’ombe, kitengo cha usalama barabarani, alipokuwa akizungumza katika kipindi cha siku mpya kinachorushwa na Radio Boma Hai FM.
Amesema kuwa ukaguzi wa vyombo vya moto mara kwa mara humwezesha dereva kutumia chombo chake kwa kujiamini na kusaidia kuepusha madhara kwa watumiaji wengine wa barabara.
Aidha, ameongeza kuwa ukaguzi wa chombo cha moto unapaswa kufanyika mara kwa mara bila kujali kama dereva atasafiri umbali mrefu au mfupi, ili kuhakikisha usalama wake na wa watumiaji wengine wa barabara.
Sajenti Ramadhani amewapongeza madereva wengi ambao wamekuwa wakikagua vyombo vyao mara kwa mara na kwamba ajali nyingi zinazotokea barabarani si zote zinatokana na ubovu wa magari, bali baadhi husababishwa na madereva kutokuzingatia sheria za usalama barabarani pamoja na kutokuwa makini wanapokuwa wanaendesha.