Boma Hai FM

Wananchi Hai watakiwa kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la mpiga kura

16 May 2025, 7:40 pm

Mkuu wa wilaya ya Hai Hassan Bomboko akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake(hawapo pichani) picha na Eliya Sabai

Ikiwa imebaki miezi kadhaa kufanyika kwa uchaguzi mkuu Octoba 2025 ,zoezi la uhakiki wa taarifa pamoja na kuboresha taarifa za wapiga kura katika daftari la kudumu la mpiga kura limeanza rasmi katika maeneo mbalimbali hapa nchini ikiwemo wilaya ya Hai.

Na Elia Sabai .Hai -Kilimanjaro

Mkuu wa wilaya ya Hai Hassan Bomboko amewataka wa wilaya ya Hai kujitokeza kwa wingi katika zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la mpiga kura ili waweze kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Octoba 2025.

Bomboko ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo Mei 16 2025 na kusema kwamba wananchi wote wanatakiwa kuhakiki taarifa zao kama ni sahihi na kwamba ambao hawakujiandikisha awamu iliyopita kwa sasa ni muda wao kufanya hivyo kwani ndio msingi wa uchaguzi huru na haki.

“Ndugu waandishi wa habari nimewaita kwenye mkutano huu wenye agenda moja tuu ya kuwatangazia wananchi wote wa wilaya ya Hai ,kwamba tumeanza zoezi la maboresho ya daftari la mpiga kura awamu ya pili na kwa wilaya yetu ya Hai  leo tumeanza rasmi,kwa hiyo wananchi wote ambao hawakupata fursa katika awamu ya kwanza wa kuhakiki taarifa zao, ni wajibu na wakati wao kwenda kuhakiki taarifa zao na kuona kama taarifa zao zipo sahihi.”Amesema Bomboko

Sauti ya mkuu wa wilaya ya Hai Hassan Bomboko akiwataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika kuhakiki na kuboresha taarifa zao katika daftari la kudumu la mpiga kura.

Hata hivyo Bomboko ametumia fursa hiyo kuwasihi viongozi wa dini kuwa mabalozi kwa waumini wao kwa kuwakumbusha kujitokeza katika kuhakiki taarifa zao pamoja na kuziboresha.

Sauti ya mkuu wa wilaya ya Hai akiwasihi viongozi wa dini kutumia nafasi walizonazo katika kuwakumbusha wananchi kujitokeza kuhakiki na kuboresha taarifa zao.

Kwa upande wao wananchi waliojitokeza kwa ajili ya kuhakiki taarifa zao wamesema kuwa watakuwa mabalozi wazuri kwa wale wote ambao bado hawajajitokeza kuhakiki pamoja na kuboresha taarifa zao katika daftari la kudumu la mpiga kura ili ifikapo Octoba 2025 waweze kutimiza haki yao ya kikatiba kwa kumchagua kiongozi wanaemtaka.

Mwananchi aliyejitokeza katika kituo cha Kantini Bomani kilichopo Boma’ngombe kwa ajili ya kuhakiki taarifa zake katika daftari la kudumu la mpiga kura( picha na Eliya Sabai)

Zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la mpiga kura awamu ya pili wilayani Hai limeanza leo Mei 16 na linatarajiwa kukamilika Mei 22 2025.