TYC yawanoa vijana Kilimanjaro kuhusu umiliki wa ardhi
18 August 2024, 9:55 am
Tyc wameendelea kuwajengea uwezo vijana mbalimbali nchini Tanzania katika mikoa minne ambayo mradi wa Boresha maisha kwa vijana unatekelezwa.
Na Elizabeth Mafie
Shirika la Tanzania Youth Coalition (TYC) limeendelea kuwajengea uwezo vijana mbalilmbali katika mkoa wa Kilimanjaro kupitia mradi wa Boresha maisha wenye lengo la kuwaongezea uwezo katika kuendesha mashirika yanayoongozwa na vijana hao,kuweza kukabiliana na ukatili wa kijinsia , pamoja na kuwa na uelewa kuhusu umiliki wa aridhi na namna bora ya kutumia aridhi hiyo.
Shirika hilo limefanya mafunzo kuhusu mifumo ya kisheria pamoja na haki za umiliki wa ardhi August 15 2024 katika ukumbi wa chuo cha uhamiaji Moshi mjini mkoani Kilimanjaro na kihudhuriwa na vijana wapatao ishirini na tano wanaotoka katika vikundi mbalimbali.
Yahaya Kitogo ambae ni mratibu wa mradi wa Boresha Maisha ya vijana nchini Tanzania amesema wamekuwa na mafunzo endelevu kuhusu mada mbali mbali kwa vijana ambao wananufaika na mradi huo katika mkoa wa Kilimanjaro na katika mkoa wa Mwanza, Dodoma na Iringa na kwamba kwa sasa wameona ni vyema vijana hao kujengewa uwezo kuhusu mifumo ya kisheria pamoja na haki za umiliki wa ardhi nchini Tanzania kwa kuwa vijana hao wanajihusisha na kilimo hivyo ni vyema kujua sheria zinasemaje na namna ya kuweza kuwa wamiliki wa ardhi.
Kitogo ameongeza kuwa shirika hilo linalenga kuwafikia vijana mia tano kwa mkoa wa Kilimanjaro na kwa nchi nzima wanatarajia kuwafikiwa vijana 11,606 kupitia makundi mbalimbali ya vijana wakulima na wanaojihusidha na shughuli za ubunifu na kwamba katika mwaka huu wa pili wa utekelezaji wa mradi wamefanikiwa kuwafikia vijana 1788 ikiwemo vikundi vya vijana 100 katika mikoa ambayo mradi huo unatekelezwa.
Nae mratibu wa mradi huo katika mkoa wa Kilimanjaro Stanley Jeremia amesema kwa kuwa ni ngumu kuwafikia vijana wengi kwa wakati mmoja wameona ni vyema kuwajengea uwezo viongozi wa vikundi na masharika ambapo wao wanakwenda kuwapatia elimu wanachama wao kwenye vikundi na kwenye taasisi.
Aidha wakili na mtaalamu wa masuala ya ardhi kutoka Tala ambae alikuwa mkufunzi wa mafunzo hayo Masalu Luhula amesema kuwa vijana wengi hawana uelewa wa kutosha kuhusu utawala wa ardhi hivyo anaamini kupitia mafunzo hayo vinaja hao watapata kujua zaidi kuhusu utawala wa ardhi na kuitumia vizuri kwa kupitia vikundi au mtu mmoja mmoja kwa lengo la kuchangia katika uchumi.
Kwa upande wao wanufaika wa mradi huo Joseph Godfrey na Veronica lema wamesema kuwa shirika la Tanzania Youth coalition(TYC) limekuwa msaada mkubwa kwa vijana kutokana na mafunzo mbalimbali ambayo wamekuwa wakipatiwa kwani yamefanya vikundi vyao viwe na uelewa wa maswala mbalimbali kama vile usawa wa kijinsia,namna ya kufanya kilimo chenye tija,namna ya kumiliki ardhi na kuitumia na kwamba vijana wengine wanapaswa kujiunga na vikundi ili kupata fursa hapa nchini.