Bodi ya maji Uroki Bomang’ombe yapeta, wadau waridhishwa na huduma
9 April 2024, 9:20 pm
Bodi ya maji Uroki Bomang’ombe wafanya mkutano na wadau wa maji,waeleza mafanikio ndani ya miaka mitatu,wadau wakiri huduma za maji zimeboreshwa.
Na Elizabeth Mafie
Bodi za maji za wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro zimetakiwa kuhakikisha kuwa zinafanya kazi kwa weledi na ufanisi na kuendelea kutoa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi ili kuondoa malalamiko kuhusu maji kwani kwa kufanya hivyo ni utekelezaji wa ilani inayotekelezwa hapa Nchini.
Hayo yamesemwa na mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Hai Wan’guba Maganda alipomwakilisha mkuu wa wilaya ya Hai Amiri Mkalipa katika mkutano wa Bodi ya maji Uroki Bomang’ombe na wadau wa maji uliofanyika April 9 2024 katika ofisi kuu za bodi hiyo zilizopo kata ya Romu.
Maganda amesema kuwa wakati wa kampeni za mwaka 2020 kilio kikubwa cha wananchi wa wilaya ya Hai ilikuwa ni upatikanaji wa maji safi na salama ,lakini kwa sasa kutokana na kazi kubwa wanayofanya Bodi ya Maji Uroki Bomang’ombe na kwamba bodi hiyo imewakomboa na adha ya muda mrefu ya kukosekana kwa maji hakuna changamoto hiyo hivyo ni vyema kuendelea kufanya vizuri zaidi.
“Wakati ule napiga kampeni ,katika vipaumbele vya kampeni ile vitu tulivyikuwa tunavikazia ni barabara,elimu, umeme afya na maji ,lakini niwe mkweli katika vitu nlikuwa naongea kwa kigugumizi ni maji,shida iliyokuwa ya maji kwenye kata ya Romu , shida tuliyokuwa tunaipata kwenye kata zile tatu za Bomang’ombe hasa kata ya Muungano shida naijua mimi, lakini leo tunaweza kuoga muda wowote tunaotaka ,serikali ya Dr Samia,wote tunajua imekusudia kuondoa adha kwa wanachi wake katika haya mambo matano,na hasa maji kwa kauli mbiu kwamba kumtua mama ndoo kichwani.”Amesema Maganda
Kwa upande wake mwenyekiti wa bodi hiyo Elisante Kimaro amesema kuwa Bodi ya maji Uroki Bomang’ombe ina mafanikio mbalimbali tangu bodi hiyo ilivyoingia madarakani mwaka 2021 na kwamba kipindi hicho hali ya huduma ilikuwa hafifu na isiyoridhisha kwani upatiakanaji wa maji safi na salama katika upande wa tambarare ilikuwa changamoto kutokana na mgao wa maji,lakini kutokana na mipango thabiti ya bodi hiyo kwa kushirikiana na Ruwasa Mkoa pamoja na wilaya kwa kipindi chote cha miaka mitatu hadi sasa wameboresha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wilaya ya Hai kwa kupata maji pamoja na kuongeza idadi ya wateja kutoka elfu kumi na moja mia tisa na tisini na nne lakini kwa sasa wana zaidi ya wateja elfu tatu.
Nae Mkuu wa wilaya ya Hai Amiri Mkalipa amesema kuwa anawapongeza Bodi ya maji Uroki Bomang’ombe kwa kusimamia vizuri fedha mradi wa maji za Mh Rais Dr Samia Suluh Hassan chini ya Ruwasa kwani Hai ilikuwa na changamoto kubwa ya maji na kwa sasa hakuna changamoto hiyo na kwamba tayari wamesaini mkataba wa milioni mia tisa tisini na saba kwa ajili ya sadala pamoja na kuongeza nguvu Bomang’ombe hivyo muda sio mrefu maji yatakuwa yanatosheleza wakaazi wote wa Hai na kuwakumbusha wananchi kutofanya shughuli za kibinadamu katika vyanzo vya maji na badala yake watunze vyanzo hivyo pamoja na kupanda miti kwa wingi.
Akizungumza kuhusu mafanikio meneja wa bodi hiyo Mhandisi Anold Mbaruku amesema kuwa kwa kipindi cha miaka mitatu Bodi hiyo kwa kutumia fedha zake za ndani imefanikiwa kujenga chanzo kipya cha maji cha Salim Karenga ambacho kimeongeza upatikanaji wa maji katika vijiji vya Mamba ,Uswaa pamoja na Roo ,pamoja na kupeleka maji Kimaroroni sehemu ambayo haikuwahi kupata maji tangu nchi ipate uhuru.
Nao wadau na bodi ya maji Uroki Bomang’ombe wameishukuru bodi hiyo kwa namna walivyoboresha huduma zao pamoja na upatikanaji wa maji safi na salama na ya uhakika kwani walikuwa wakipata adha kubwa kutokana na kukosekana kwa maji.