Bodi ya maji Losaa Kia yafanya uchaguzi,waweka mikakati
27 March 2024, 7:04 pm
Bodi ya maji Losaa Kia yapata viongozi wapya,waomba ushirikiano.
Na Edwine Lamtey
Wananchi wanaoishi karibu na vyanzo vya maji wametakiwa kuvilinda na kuvitunza vyanzo hivyo ili kusaidia upatikanaji wa huduma hiyo na itakayokuwa toshelevu katika maeneo yote ikiwemo yale ya ukanda wa tambarare.
Wito huo umetolewa na Vumilia kweka mwenyekiti mpya wa bodi ya maji Losaa kia, wakati akitoa neno la shukrani baada ya kuchaguliwa kuiongoza bodi hiyo na kusema kuwa bodi hiyo itaendelea kutoa elimu ya utunzaji wa mazingira kama njia mojawapo ya kutatua changamoto ya maji kwa baadhi ya maeneo yanayohudumiwa na bodi hiyo.
Aidha pia mwenyekiti huyo amewataka watendaji wa bodi hiyo kuendelea kuwajibika na kuwatumikia wananchi wanaowahudumia na kutatua changamoto kwa haraka pindi zinapotokea kwani huduma ya maji ni huduma msingi na muhimu katika jamii.
“Nawashukuru mmenichagua na naenda kuendeleza kazi ambayo ilikuwa imekwisha anzwa hivyo niwaombe wote tushirikiane; madiwani na wenyeviti mliopo hapa naomba imani yenu hakuna atakayekosa kura kisa tu hakuna kilula ama kilula hakifanyi kazi katika eneo lake maana natambua azma ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kumtua mama ndoo kichwani”. Alisema Vumilia Kweka.
Naye msimamizi wa uchaguzi huo Mhandisi Benedict amesema kuwa uchaguzi huo ni takwa la kisheria na hivyo wote waliopata nafasi hiyo wanapaswa kufanya kazi kwa maslai mapana ya jamii wanayoihudumia.
Waliochaguliwa katika bodi hiyo mpya ni Vumilia kweka ambaye mwenyekiti, Luka laizer akishinda nafasi ya makamu huku wajumbe wengine wakiwa ni Rose Kimaro, Saraphina Mmasy, Raymond Anania na Kandata Kimaro.