Makamu wa Rais azindua mradi wa maji Hai, mbunge Saashisha awasilisha kero
20 March 2024, 7:23 pm
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amezindua mradi mkubwa wa maji Hai, mradi ulioondoa changamoto ya maji kwa wakazi wa wilaya hiyo.
Na Edwine Lamtey
Serikali imesema itaendelea kuhakikisha kuwa huduma ya maji nchini inapatikana kwa ukaribu na unafuu badala ya wananchi kutembea umbali mrefu kwenda kutafuta huduma hiyo.
Hayo yamesemwa na Makamu wa ra3is wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango wakati akizindua mradi wa maji Kikafu – Bomang’ombe ambao kukamilika kwake kumesaidia kuondoa tatizo la maji kwa wakazi wa mamlaka ya mji wa Hai pamoja na wale walio pembezoni.
Amesema kuwa lengo la serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kuwa inamtua mama ndoo kichwani kwa kuhakikisha kuwa huduma ya maji inapatikana katika maeneo yao badala ya wananchi kutembea umbali mrefu.
Awali akisoma taarifa ya ujenzi wa mradi wa maji Kikafu – Bomang’ombe, meneja wa RUWASA mkoa wa Kilimanjaro Eng. Munis amesema kuwa serikali ilitenga kiasi cha shilingi Bilion 3.39 ambapo hadi kukamilika kwake jumla ya bilion 2.8 ndizo fedha pekee zilizotumika.
Kwa upande wake mbunge wa jimbo la Hai Saashisha Mafuwe ameishukuru serikali kwa kugharamia mradi huo ambao tija yake tayari imekwishaonekana kwa wananchi ambao walikuwa wahanga wakubwa.
Katika hatu nyingine mbunge Saashisha pia amekumbushia upanuzi wa barabara ya Arusha hadi Holili, ujenzi wa barabara ya Bomang’ombe TPC na ujenzi wa barabara ya Sadala – Lemira bila kusahau ujenzi wa soko la kisasa Kwa Sadala.
Akijibu kuhusiana na hoja hizo Makamu wa rais Dkt. Mpango amesema kuwa serikali imekwishatenga kiasi cha shilingi bil 11.2 za ujenzi wa soko Kwa Sadala na ameagiza TAMISEMI kuharakisha juu ya utoaji wa fedha hizo, huku katika ujenzi wa barabara ya Sadala Lemira, Bomang’ombe hadi TPC akiziagiza Tarura na Tanroad kila mmoja kushughulika na kipande kilicho katika mamlaka yake huku Wizara ya Ujenzi ikitakiwa kuhakikisha inaweka mpango wa uendelezaji wa barabara kuu ya Arusha hadi Holili na kuhakikisha inakuwepo kwenye bajeti ijayo.
Pamoja na hayo ameiagiza TAMISEMI kuhakikisha kuwa inafanya tathmini katika suala la uchakavu wa miundombinu ya shule ili serikali iweze kutatua kero hiyo iliyowasilishwa na mbunge Saashisha Mafuwe.