Wanawake waomba kujengewa kituo cha kulelea watoto kazini
12 March 2024, 2:06 pm
Kutokana na changamoto za malezi ya watoto zinazowakabili wanawake watumishi katika taasisi mbalimbali, watumishi hao wameomba kujengewa kituo cha kulelea watoto.
Na Elizabeth Mafie
Wanawake watumishi kutoka taasisi mbalimbali ikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) kupitia shirika lake la Msamaria Mwema(GSF) wameomba kuwekewa mazingira mazuri ya kufanya kazi kwa kujengewa kituo maalum cha kulelea watoto wao pindi wanapomaliza likizo ya uzazi ili waweze kuwa karibu na watoto wao wawapo kazini kwa kupata muda wa kunyonyesha watoto wao badala ya kurudi nyumbani mchana kunyonyesha.
Wamesema baada ya likizo ya miezi mitatu kuisha wamekuwa wakikabiliana na changamoto mbalimbali za usafiri hasa wanapotakiwa kurudi nyumbani mchana kunyonyesha watoto na kwamba muda wa kwenda na kurudi hautoshi hivyo kufanya kazi katika mazingira magumu.
Ombi hilo limetolewa na Mkuu wa Idara ya Rasilimali Watu wa hospitali ya KCMC Dorah Olotu mbele ya Katibu Mkuu Mtendaji wa Shirika hilo na Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali ya KCMC Profesa Gileard Masenga wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake duniani ambayo yamefanyika jana katika ukumbi wa Kuringe, Manispaa ya Moshi.
Olotu amesema kuwa shirika hilo lina wanawake zaidi ya 1,118 ambao umri wao bado ni kwa kuzaa hivyo akaliomba shirika hilo kuona umuhimu wa kujenga kituo maalum kwa ajili ya watoto wao ili pindi wanapotaka kwenda kunyonyesha iwe ni rahisi.
Ameongeza kuwa wazo la serikali la mama kutoka kazini saa saba na kwenda kunyonyesha mtoto wake linakuwa halifanikiwi, na wameona ni changamoto na ni kilio cha wanawake wengi kutokana na wasichana wanaowasaidia kulea watoto hao baadhi yao hutoroka na wengine huondoka kwa kushtukiza huku mwanamke huyo akitakiwa kwenda kazini.
Ameeleza kuwa kuna changamoto nyingi ambazo zinahusiana na malezi ya watoto, hivyo kama Katibu Mtendaji wa shirika la Msamaria Mwema akiwajengea kituo cha kulelea watoto, watoto wao watapata huduma nzuri na kwamba wafanyakazi watatulia kazini, na kufanya kazi kwa bidii pamoja na kuongeza ufanisi huku watoto wakiendelea kuwa na afya njema.
Akijibu ombi la wanawake hao, Prof. Masenga amesema kuwa lipo eneo ambalo lilitengwa na shirika hilo hivyo wataangalia namna ya kupata rasilimali fedha kwa ajili ya kuanzisha kituo hicho maalum kwa ajili ya watumishi wanawake wa shirika hilo.