Mvua kubwa yaua watatu Same
16 January 2024, 11:58 am
Kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha wilayani Same Mkoani Kilimanjaro na zimesababisha madhara katika miundombinu ya barabara pamoja na kusababisha watu kupoteza maisha.
Na Elizabeth Mafie
Watu watatu wamefariki Dunia Wilayani same Mkoani Kilimanjaro kwa kufukiwa na nyumba na mmoja kusombwa na maji kufuatia mvua kubwa iliyonyesha mapema mwezi huu.
Akizungumza na waandishi wa habari Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilayani Same Kaslida Mgeni ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya hiyo ya Same amesema mvua kubwa iliyonyesha kuanzia tarehe 07-11 January hii hususani huko Same mashariki ilileta maafa makubwa kwa wananchi wa maeneo hayo.
Kaslida amesema pamoja na mvua hiyo kusababisha vifo hivyo pia imesababisha nyumba zaidi ya 15 kuanguka huku ekari zaidi ya 400 za wakulima wa mpunga kufukiwa sambamba na miundombinu ya umwagiliaji kuharibiwa vibaya
Aidha Kaslida amesema mvua hizo zimekata mawasiliano ya barabara zaidi ya saba zinazounganisha wananchi wa Kata za Vuje,Bombo,Mtii na Lugulu huku akisema daraja linalounganisha wananchi wa Kata za tambarare Same mashariki lilizolewa na mvua hizo.
Mgeni amewataka wananchi wilayani hapo hasa wananchi wa ukanda wa juu kushirikiana na shirika la Floresta Tanzania ambalo linajihusisha na utunzaji wa mazingira katika kupanda miti ya kutosha ilikuweza kuyalinda mazingira.
Hata hivyo jamii imetakiwa kuendelea kuchukua tahadhari ya mvua kubwa zinazoendelea kunyesha kwenye maeneo mbalimbali hapa Nchini kwani mvua hizo zimekuwa zikinyesha juu ya wastani.