Wanafunzi wasiokuwa na sare kuendelea na masomo
5 January 2024, 11:23 pm
Zikiwa zimebaki siku chache shule za msingi na sekondari kufunguliwa hapa nchini mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu atoa wito kwa wakuu wa shule.
Na Elizabeth Mafie
Wito umetolewa kwa wakuu wa shule za msingi na sekondari katika mkoa wa Kilimanjaro kutokuweka vikwazo kwa wanafunzi wanaotarajia kurejea mashuleni siku za hivi karibuni na kwamba ni marufuku kumzuia kuendelea na masomo mwanafunzi ambae hana sare.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Nurdini Babu hii leo, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake ambapo amesema suala la mwanafunzi kutokua na viatu au sare za shule lisimfanye mwalimu kumrudisha mwanafunzi nyumbani kwa kuwa mengine yanazungumzika mwanafunzi akiwa darasani.
Hata hivyo, amesema ni marufuku wakuu wa shule kuendesha michango isiyo kuwa ya lazima mashuleni na kwamba kama kuna michango upo utaratibu wa kufuatwa.
Pamoja na mambo mengine, ametoa rai kwa wazazi na walezi wote katika mkoa wa Kilimanjaro, kuhakikisha wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza wote wanaripoti shuleni bila kisingizio chochote kwa kuwa serikali imefuta ada mashuleni.
Babu amesema kuwa jumla ya wanafunzi 36, 570 wakiwemo wavulana 18,013 na wasichana 18,557 ambao walifaulu mitihani yao ya darasa la saba wote watapata nafasi za kujiunga na kidato cha kwanza katika shule mbalimbali walizochaguliwa .
Hata hivyo, Babu amewakumbusha wazazi na walezi kuchangia chakula mashuleni ili watoto waweze kupata chakula wakiwa shuleni na kwamba ni jukumu la kila mzazi kutekeleza wajibu huo.