Hospitali Siha yakabidhiwa vifaa tiba na magari matatu
22 December 2023, 2:20 pm
Vifaa tiba pamoja na gari vilivyokabidhiwa katika hospitali ya wilaya ya Siha (picha na Elizabeth Mafie)
Hospitali ya wilaya ya Siha imekabidhiwa vifaa tiba pamoja na magari vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni mia tisa.
Na Elizabeth Mafie
Ambulance mbili kwaajili ya kubebea wagonjwa na gari moja ya Mtabibu Mkuu pamoja na vifaa vyenye thamani zaidi ya shilingi Milioni mia tisa vimekabidhiwa katika hospitali ya wilaya ya Siha huku wataalamu wa sekta hiyo ya Afya wakitakiwa kuongeza ufanisi zaidi kwa kutoa huduma bora na zenye uhakika kwa wananchi [wagonjwa] kwani uwepo wa vifaa pekee hautoshi bali huduma bora za kimatibabu.
Akizungumza katika zoezi la uzinduzi rasmi wa huduma ya upimaji wa Magonjwa ya moyo linaloendelea kufanyika hospitalini hapo chini ya Taasisi ya Moyo ya JKCI Naibu waziri wa afya Dk Mollel ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Siha amesema sekta ya Afya inahitaji umakini hivyo madaktari waongeze ufanisi wananchi wapatiwe huduma kwa wakati kuepukana na madhara yatokanayo na maradhi.
Aidha ameongeza kwa kusema JKCI watawasaidia wananchi kutibiwa,kuhamasisha watu kuishi maisha salama, zaidi kuwajengea uwezo Madaktari wa Wilaya kusaidia kuwa na utambuzi wa haraka pindi anapojitokeza Mgonjwa wa Moyo lengo ikiwa ni kupata rufaa ya haraka kabla ya madhara yatokanayo na ugonjwa huo.
Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Siha Dkt Haji Mnasi pamoja na Mwenyekiti Halmashauri ya Wilaya ya Siha Dankan Benjamin Urrasa,wamesema wamepokea kwa furaha huduma ya JKCI na wananchi watumie fursa hiyo .Aidha vifaa vilivyo tolewa na Mh Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania vitakuwa na mchango mkubwa kwenye sekta ya Afya.
Dkt Delila Kimambo ambaye ni daktari bingwa JKCI amesema bado zoezi linaendelea hivyo wananchi waendelee kujitokeza kupata vipimo.
Hata hivyo siku mbili za vipimo vya ugonjwa Moyo zimeongezwa, watu 307 hadi sasa wamefanyiwa vipimo huku watu 37 wakipatiwa rufaa ya kwenda kutibiwa kulingana na matokeo ya vipimo kuonyesha kuwa wanahitaji matibabu zaidi.