HRT watoa msaada kwa wanafunzi wenye uhitaji
21 December 2023, 9:52 pm
Chama cha ushirika wa akiba na mikopo Hai Rural Teachers SACCOS (HRT) wilayani Hai mkoani Kilimanjaro kimetoa msaada wa sare za shule kwa wanafunzi wenye uhitaji kutoka shule 16 za wilaya ya Siha.
Na Elizabeth Mafie
Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo (Hai Rural Teachers SACCOS (HRT) kilichopo wilayani Hai mkoa wa Kilimanjaro kimekabidhi msaada wa sare za shule kwa wanafunzi 55 wanaoishi katika mazingira magumu kutoka katika shule 16 za wilaya ya Siha huku wazazi na walezi wilayani humo wakitakiwa kuwasimamia watoto wao shuleni ili waweze kusoma kwa bidii na kuweza kutimiza ndoto zao.
Msaada huo wenye thamani ya shilingi milioni mbili umekabidhiwa katika eneo la shule ya msingi Sanya Juu na Mwenyekiti wa chama hicho Mwalimu Alex Warioba ambapo amesema matendo hayo ya huruma waliyofanya ni sehemu ya misingi ya vyama vya ushirika na kwamba wana misingi saba na msingi mmojawapo ni kuijali jamii na kwamba watoto hao wapelekwe shule kwani shule zimejengwa, madawati ya kutosha na wao wameamua kutoa sare hizo.
Amesema kuwa wamegusa shule 16 ambapo watoto 55 wanaotoka shule tofauti tofauti za wilaya ya siha, ambao wanasoma darasa la kwanza hadi la sita, wameshonewa sare za shule.
Kwa upande wake meneja wa chama hicho Upendo Lyatuu amesema kuwa chama hicho kina utaratibu wa kila mwaka kutenga kile wanachokipata kama faida kwenye chama kwa ajili ya kuijali jamii wana utaratibu wa kupokeza katika wilaya mbili kwa kuwa wanachama wao wanatoka katika wilaya ya Hai pamoja na Siha hivyo mwaka jana walitoa wilaya ya Hai na mwaka huu wametoa wilaya ya Siha na waliona ni vyema kuwagusa wale wanafunzi ambao wanatoka katika mazingira magumu kwa kuwashonea sare za shule ili nao waweze kujisikia vizuri kama wanafunzi wengine.
Upendo amewaomba wanafunzi hao kusoma kwa bidiii kwani wao kama chama watafurahi kuwaona wanafunzi hao wameshasoma na kufanikiwa kuwa kwenye ajira na wamejiunga na kuwa wanachama wa chama hicho.
Amesema Chama hicho kina jumla ya wanachama wapatao 2560 kwa sasa ambao wanatoka katika wilaya za Siha na Hai.
Kwa upande wao wazazi wa watoto hao na mwalimu Frank Mariki pamoja wanafunzi waliopatiwa sare hizo walishukuru chama hicho cha akiba na mikopo kwa kuwajali wanafunzi wao ambapo wamesema wanafunzi hao wanaishi katika mazingira magumu kwani hawana namna ya kujitetea kifedha.