JKCI wasogeza matibabu ya kibingwa Kilimanjaro
19 December 2023, 7:42 pm
Taasisi ya moyo Jakaya Kikwete ( JKCI ) yaanza kutoa huduma za matibabu ya kibingwa katika mkoa wa Kilimanjaro.
Na Elizabeth Mafie
Wananchi mkoa wa Kilimanjaro na mikoa jirani wameanza kupatiwa huduma na matibabu ya kibingwa ya ugonjwa wa moyo katika hospitali ya wilaya ya Siha kupitia huduma ya tiba mkoba ya Mh Dkt Samia Suluh Hassan inayoendeshwa na Taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) iliyoanza rasmi disemba 18 na inatarajiwa kukamilika disemba 22 2023.
Akizungumza kuhusiana na huduma hiyo mkuu wa kitengo cha uhusiano na mawasiliano taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete Anna Mkinda amesema kuwa taasisi hiyo imekuwa ikipokea wagonjwa wengi wakiwa katika hali mbaya kutokana na tatizo kutokugundulika mapema hivyo ili kukabiliana na changamoto hiyo taasisi hiyo imeamua kuwafata wananchi katika maeneo yao kupitia tiba mkoba ya Mh Dkt Samia Suluhu Hassan na kwamba ni katika jitihada kuiunga serikali ya awamu ya sita mkono kwani lengo la serikali ni kuhakikisha kila mwananchi anafikiwa na huduma za kibingwa.
Kwa upande wake Theophil Ludovick ambaye ni daktari bingwa wa watoto kutoka taasisi hiyo amesema kuwa wanafanya uchunguzi wa magonjwa ya moyo kwa watoto na kwamba zipo dalili mbalimbali ambazo zinaweza kuhashiria ugonjwa wa moyo kwa watoto ikiwepo kutoka jasho hata ikiwa hajacheza ,vikohozi vya mara kwa mara ,kudhohofu mwili na hata wakati mwingine kuvimba miguu.
Aidha Dr Theophil ameongeza kuwa ni vyema jamii ikawa na utaratibu wa kupima afya za watoto wao mara kwa mara kwani itasaidia kuondokana na tatizo hilo mapema tofauti na kugundulika kwa kuchelewa kwani huleta athari zaidi.
Nae Mganga mkuu wa wilaya ya Siha Dr Pascal Mboto amesema kuwa lengo la taasisi hiyo kuwa katika hospitali hiyo ni kusogeza huduma kwa wananchi na kwamba huduma hiyo imekuwa na msaada mkubwa katika wilaya hiyo na wilaya za jirani kwani wanatoa huduma za kibingwa za magonjwa ya moyo kwa watoto na watu wazima na endapo mgonjwa ataonekana anatakiwa matibabu zaidi upo mfumo wa rufaa ambao taasisi hiyo wameandaa na kusema kuwa ni vyema wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro kujitokeza kwa wingi ili kunufaika na fursa hiyo.
Hata hivyo kwa upande wa wananchi waliopatiwa huduma hiyo Issa Lipongo kutoka wilaya ya siha amesema kuwa amefurahia huduma hiyo kwani amepata huduma zote na vipimo vya magonjwa ya moyo na imekuwa manufaa kwa wananchi kwani huduma hiyo huwa inapatikana Dar es saalam lakini taasisi hiyo imeamua kuwafata walipo jambo ambalo linawapunguzia gharama .