KCMC yasherehekea sikukuu na watoto wenye saratani
16 December 2023, 9:36 pm
Katika kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka, KCMC imefanya hafla kwa ajili ya kusherehekea na watoto wenye changamoto ya saratani pamoja na wazazi wao.
Na Elizabeth Mafie
Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) iliyopo Moshi mkoani Kilimanjaro kupitia kitengo cha utafiti KCRI imeandaa hafla ya chakula cha pamoja na watoto ambao ni wagonjwa wa saratani waliolazwa hospitalini hapo na wazazi wao lengo likiwa ni kuonesha upendo katika kipindi hiki cha sikukuu za mwisho wa mwaka.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo Mkurugenzi Mkuu wa hospitali ya KCMC Prof. Giliad Masenga amesema hospitali hiyo kupitia kitengo cha saratani huwa wanatoa tiba kwa watoto wenye saratani bila malipo na kwamba serikali ni miongoni mwa wadau wakubwa wanaochangia ili kuwatibu watoto hao kwa kutoa vifaa tiba na madawa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utafiti KCMC /KCRI Prof. Blandina Mmbaga, amesema wamekuwa wakishiriki hafla ya chakula na watoto hao wenye saratani ambao wamelazwa hospitali hapo kwa muda mrefu kutokana na aina ya matibabu wanayopatiwa msimu huu wa Christmas ili kuwapa tabasamu.
Hata hivyo amesema jamii ikieleweshwa vizuri na kuzijua dalili zinazosababisha saratani kuna uwezekano mkubwa wa kuzuia mapema magonjwa ya saratani hasa kwa watoto na watu wazima.