Wananchi Siha wahimizwa kujitokeza kupata huduma za kibingwa
15 December 2023, 9:45 pm
Wananchi wilayani Siha Mkoani Kilimanjaro wahimizwa kujitokeza kwa wingi kupata huduma za kibingwa na matibabu ya ugonjwa wa moyo .
Na Elizabeth Mafie
Mganga mfawidhi wa hospitali ya wilaya ya Siha Dkt Nsubili Mwakapeje amewataka wananchi na wakaazi wa wilaya hiyo kujitokeza kwa wingi katika huduma ya kibingwa za upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo kutoka taasisi ya moyo Jakaya Kikwete (JKCI) inayotarajiwa kufanyika Disemba 18-22,2023 zitazotolewa katika hospitali ya wilaya ya Siha.
Dkt Mwakapeje ameyasema hayo hii leo katika kikao cha pamoja na wananchi kilichofanyika hosptalini hapo wanaopata huduma za magonjwa ya presha na sukari katika hospitali ya wilaya hiyo .
Amesema kutokana na mkakati wa serikali wa kuwasogezea huduma wananchi ili kupunguza gharama za kufuata huduma mbali na maeneo yao kupitia mkoba Taasisi ya moyo Jakaya Kikwete imeamua kufika wilayani Siha ili kutoa huduma za kibingwa za upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo.
Ameongeza kwa kusema kuwa Mbunge wa jimbo la Siha ambae pia ni naibu waziri wa afya Dkt Godwin Mollel ameonyesha kwa vitendo kuwa anawajali wananchi wa wilaya ya Siha kwa kuwasogezea huduma za kibingwa karibu.
Nae mmoja wa wananchi wa wilaya hiyo Upendo Joseph amesema kuwa huduma hiyo ni fursa kwao kwani hosptali inayotoa huduma hiyo ya magonjwa ya moyo ni mbali na makaazi yao hivyo hawawezi kumudu gharama lakini kwa kufika katika wilaya hiyo imekua msaada kwao.