Dc Mkalipa awataka vijana kuacha ulevi uliopitiliza
14 December 2023, 1:24 pm
Mkuu wa wilaya ya Hai Amir Mkalipa amewataka vijana katika vijiji vya kata ya Machame Magharibi kuacha unywaji wa pombe uliopitiliza kwani vijana ni nguvu kazi ya Taifa.
Na Elizabeth Mafie.
Serikali Wilayani Hai Mkoani Kilimanjaro imewataka vijana kuacha tabia ya ulevi uliopitiza huku ikiwataka wananchi kupiga vita vitendo vya ukatili wa kijinsia na badala yake kuwa mabalozi wazuri wa uhifadhi wa mazingira.
Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Nshara, alipokuwa akifanya ziara ya kuzungumza na wananchi na kusikiliza kero zinazowakabili wananchi wa kata hiyo, Mkuu wa wilaya hiyo Amiri Mkalipa amesema ni vyema vijana kupambana ili kusaidia familia zao na kuachana na ulevi kwani huleta umaskini katika familia .
Mkalipa ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya usalama ya Wilaya hiyo amesema wapo vijana wanalewa kuanzia asubuhi mpaka jioni na hawafanyi shughuli yoyote ya uzalishaji shughuli za uchumi hivyo serikali na taifa halitaweza kuvumilia.
Hata hivyo Mkalipa amewaonya wale wote wanaofanya vitendo vya ubakaji na ulawiti na huku wazee wakimalizana kwa jani aina ya sale ambapo amesema serikali haitawavumilia na itachukua hatua kali na madhubuti kwa vijana na wazazi watakaojihusisha na ukatili huo.
Hata hivyo amewatahadharisha vijana na wale wote wanaotukana hovyo katika jamii kuacha mara moja na kusema kuwa watachukuliwa hatua za kinidhamu ikiwa ni pamoja na kuwapeleka kwenye vyombo vya sheria.
Kwa upande wake mwenyekiti wa kijiji cha Nshara Warinton Kwayu amemshukuru mkuu wa Wilaya hiyo kwa kutembelea kijiji hicho na kuzungumza na wananchi na kusema kuwa maelekezo yote yaliyotolewa na serikali yatafanyiwa kazi.
Mmoja wa wananchi Lodvick Massawe amesema kuwa mkuu huyo amewahamasisha mambo mbalimbali ikiwemo kuachana na ukatili wa kijinsia na wao kama wananchi wamepokea kauli za serikali.