Diwani awatuliza wananchi wenye hasira kali
10 December 2023, 6:20 pm
Wananchi wa kijiji cha mkombozi wataka kubomoa nyumba ya mwananchi mmoja anayedaiwa kuvamia eneo la kijiji.
Na Elizabeth Mafie
Diwani wa kata ya Masama Kusini Cedrick Pangani amewataka wananchi wa kijiji cha Mkombozi Wilayani Hai mkoani Kilimanjaro kusitisha zoezi la kwenda kubomoa nyumba ya mwananchi mmoja Gabriel Kitika anayedaiwa kuvamia eneo la Kijiji hicho na kufanya shughuli za kilimo pamoja na ujenzi.
Kauli hiyo imekuja baada ya kuwepo zuio kutoka ofisi ya baraza la ardhi la kata kwamba shughuli yoyote zisifanyike hadi hapo itakapo bainika nani mmiliki halali wa eneo hilo ambapo mwananchi huyo alipuuza.
Akizungumza na wananchi wa Kijiji hicho waliokusanyika katika eneo lenye mgogoro huo ,amewataka wananchi hao kuwa wavumilivu na kusitisha zoezi hilo na kufuata taratibu za kisheria na kwamba alipata taarifa uwepo wa wananchi wa Kijiji hicho waliojikusanya kwenda kubomoa nyumba ya mwananchi huyo aliyevamia eneo la Kijiji hicho lenye ukumbwa wa ekari 10 na kuanza ujenzi kitu ambacho ni kinyume na maagizo yaliyotolewa.
Amesema kuwa mwananchi huyo baada ya uvamizi wa eneo hilo alifikishwa baraza la ardhi la kata iliyopo kwasadala na kuagizwa kuacha kufanya shughuli yoyote mpaka hapo itakapobainika nani mmiliki halali wa eneo hilo.
Hata hivyo mwananchi huyo hakutaka kufuata maagizo ya baraza na kuendelea na ujenzi ambapo wananchi walichukizwa na jambo hilo na kuamua wajikusanye kwa lengo la kubomoa nyumba hiyo ambapo Diwani huyo aliwasihi kuacha na kufuata utaratibu.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Kijiji hicho Fikiri Rezer amesema kuwa mwaka huu walifika ofisi ya aridhi ya kata na mlalamikiwa kuamriwa kutoa vielelezo lakini hakutoa na uamuzi uliotolewa ni kutokufanya shughuli yoyote katika eneo hilo mpaka hapo ufumbuzi utakapopatikana, hata hivyo baada ya mkutano huo mwananchi huyo amekubali kupeleka vielelezo alivyonavyo vinavyothibitisha umiliki wa eneo hilo katika baraza la ardhi la kata.
Nae mwenyekiti wa baraza la ardhi na nyumba kata hiyo Ally Mmbaga amesema kuwa iwapo eneo lina mgogoro hairuhusiwi mtu yoyote kufanya shughuli katika eneo hilo na atakaefanya hivyo atakuwa anatenda kosa la jinai na ameutaka uongozi wa Kijiji hicho pamoja na mwananchi huyo kupeleka vielelezo walivyonavyo ili kuweza kufahamu nani mmiliki halali.