KIA kuwekwa taa za kisasa
9 December 2023, 11:55 am
Mamlaka ya viwanja vya ndege nchini (TAA) inatarajia kufanya maboresho ya miundombinu ya viwanja vya ndege hapa nchini huku uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) ukiwekwa taa za kisasa.
Na Elizabeth Mafie
Mamlaka ya viwanja vya ndege nchini (TAA), imesema mwanzoni wa mwaka 2024, itaanza kuboresha miundombinu ya uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kwa kuweka taa za kisasa za kuongezea ndege ili kuondoa changamoto ambayo imekuwepo ya kuzimika kwa taa hizo.
Hayo yamesemwa, Desemba 8, mwaka huu na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya viwanja vya ndege nchini (TAA), Musa Mburah wakati wa ufunguzi wa wiki ya utamaduni wa usalama wa anga, ambayo yamefanyika katika kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KIA).
Amesema lengo la kuboresha miundombinu hiyo ni katika kuhakikisha wanaimarisha usalama katika viwanja vya ndege hapa nchini ambapo pamoja na mambo mengine amesema tayari wamenunua vifaa vya kisasa vya ulinzi na usalama zikiwemo mashine lakini viwezeshi ili ndege ziweze kutua kwa usalama zaidi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa uwanja wa ndege KIA, Clemence Jingu, amesema maadhimisho hayo ambayo yatafanyika kwa wiki nzima, yatalenga kutoa elimu ya usalama wa anga kwa wadau wote wanaoutumia uwanja huo wa KIA na kwamba kupitia elimu hiyo wadau hao watapata furasa ya kujua nini wanatakiwa kufanya ili ili wawe na mchango katika kuendeleza usafiri wa anga.