Highlands FM
Highlands FM
23 March 2026, 15:40

Wizara ya Afya kwa kushirikiana na UNICEF imetoa mafunzo kuhusu mwongozo wa hedhi salama kwa maafisa afya pamoja na waratibu wa afya shuleni, yakilenga kuongeza uelewa wa jamii juu ya umuhimu wa hedhi salama kwa wasichana na wanawake.
Na Anitha Adamson
Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Shirika la Kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF) wametoa mafunzo ya muongozo wa hedhi salama kwa maafisa afya na waratibu Swash shuleni, yenye lengo la kuhakikisha jamii inapata uelewa na umuhimu wa hedhi salama kwa wasichana na wanawake.
Mafunzo hayo ambayo yamewakutanisha wadau wa afya na elimu kutoka mikoa mitano ya Nyanda za Juu Kusini yamefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mkapa jijini Mbeya.
Akizungumza katika mafunzo hayo mratibu wa hedhi salama kutoka Wizara ya Afya Joy Mbogo amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo washiriki wa mafunzo ili kupata mbinu za kuhakikisha wasichana na wanawake mwanaishi katika mazingira salama hasa wakati wa hedhi na kuondoa unyanyapaa katika jamii.

Regina Mpete kutoka Unicef na Joyce Sigalla kutoka Wizara ya Elimu wamesema kuwa muongozo wa hedhi salama utawasaidia wasichana hasa waliopo shuleni kutokosa masomo wakati wa hedhi na pia kuimarisha afya ya uzazi kwa mtoto wa kike.

Akizungumza kwa niaba ya washiriki wa mafunzo hayo afisa afya mkoa wa Mbeya Nimrod kiporoza ameishukuru wizara ya afya kwa kuandaa mafunzo hayo kwani yatasaidia kuondokana na mila potofu na unyanyapaa zilizopo katika jamii kuhusu suala la hedhi.
Mafunzo hayo yanatarajiwa kuwa chachu ya mabadiliko chanya katika jamii kwa kuongeza uelewa, kuboresha huduma za afya shuleni, na kuweka mazingira wezeshi kwa wasichana kuendelea na masomo yao bila vikwazo vinavyotokana na hedhi.