Highlands FM
Highlands FM
25 February 2026, 15:35

Wataalamu wa afya na lishe wamesema kuwa kufunga na kujinyima kula kwa kipindi maalum si ibada ya kiroho pekee, bali pia kuna mchango mkubwa katika kuboresha afya ya mwili wa binadamu.
Wanasema kitendo hicho husaidia kuupumzisha mfumo wa mmeng’enyo wa chakula, kusafisha mwili na kuimarisha kinga dhidi ya magonjwa mbalimbali.
Na Asack Mwashiuya.
Wataalamu wa afya na lishe wanasema kuwa kufunga na kujinyima kula kwa kipindi maalum si ibada ya kiroho pekee, bali pia kuna mchango mkubwa kwa afya ya mwili wa binadamu.
Hayo yameelezwa na Afisa Lishe wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Lewisi Mahembe, ambaye amesema mwili wa binadamu una uwezo wa kuhifadhi chakula kama akiba.
Amefafanua kuwa wakati wa mfungo, mwili hulazimika kutumia akiba hiyo ya nishati bila kuongezewa chakula kingine, jambo linalosaidia kupunguza mafuta yasiyo na manufaa mwilini, ikiwemo lehemu.
Aidha, Mahembe amebainisha kuwa njia hiyo inaweza kuwa na manufaa zaidi kwa watu wanaotaka kupunguza uzito pamoja na wale wenye dalili au hatari ya kupata magonjwa ya moyo.
Kwa upande wao, baadhi ya wananchi mkoani Mbeya wametoa maoni mseto kuhusu suala hilo. Wapo wanaoamini kuwa kufunga kuna faida kiafya, huku wengine wakisema hawakuwa na ufahamu kuwa kujinyima kula kwa muda kunaweza kuwa na mchango chanya kwa afya ya mwili.
