Highlands FM
Highlands FM
20 June 2025, 12:16

Vijana waonywa Utoaji mimba na mapenzi ya jinsia moja ni kosa na ni hatari.
Na Samwel Mpogole
Jamii, hususan wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu, wametakiwa kuacha tabia ya kuhusika na vitendo vya utoaji mimba (abortion), kwani ni kosa kisheria, ni ukiukwaji wa haki ya kuishi kwa mtoto, na ni dhambi mbele za Mungu.
Wito huo umetolewa na Imran Mwanja, Mkufunzi kutoka Chuo cha Maendeleo ya Jamii Uyole (CDTI), wakati wa mdahalo maalum uliowakutanisha wadau mbalimbali chuoni hapo, ulioangazia masuala ya maadili, afya ya uzazi na haki za watoto.
Mwanja ameeleza kuwa vitendo vya kutoa mimba siyo tu vinaua maisha ya asiyezaliwa, bali pia vinaweza kusababisha madhara makubwa kiafya kwa wahusika, vikiwemo utasa, msongo wa akili na hata kifo.
Aidha, mkufunzi huyo amewataka vijana wa kiume na wa kike kujiepusha na mapenzi ya jinsia moja, na unaokiuka maadili ya jamii na mila zetu za Kitanzania.
Nao baadhi ya wanafunzi wa chuo hicho wameeleza namna utoaji mimba unavyosababisha maumivu ya kimwili na kisaikolojia kwa vijana, huku wakitoa wito kwa wenzao kuwa na nidhamu, kujitunza, na kutumia elimu sahihi ya afya ya uzazi.
Mdahalo huo umehitimishwa kwa wito wa pamoja kwa jamii kuwekeza zaidi kwenye elimu ya maadili, afya ya uzazi, na huduma rafiki kwa vijana, ili kupunguza mimba zisizotarajiwa na vitendo vya utoaji mimba kiholela.