Highlands FM
Highlands FM
19 June 2025, 12:18

Wazazi waonywa kuacha tabia ya kuwaachia watoto wao mikononi mwa wafanyakazi wa ndani bila uangalizi, hali inayochochea ukatili dhidi ya watoto
Na Samwel Mpogole
Jamii imetakiwa kuacha vitendo vya ukatili dhidi ya watoto ili kuwawezesha kutimiza ndoto na malengo yao katika maisha, huku wazazi na walezi wakisisitizwa kuwajibika ipasavyo kwa kuwa karibu na watoto wao badala ya kuwaachia malezi kwa wafanyakazi wa ndani au watu wengine bila uangalizi wa karibu.
Wito huo umetolewa na Catherine Mlaponi, Mkufunzi wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Uyole ambaye pia ni Mratibu wa Dawati la Jinsia, wakati wa mdahalo maalum wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika uliofanyika chuoni hapo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo hicho Bw. Silivesta Mwambene, amesema mdahalo huo umetumika kama jukwaa la kutoa elimu kwa vijana kuhusu haki za watoto pamoja na kuwajengea uwezo wa kupinga ukatili katika jamii zao.
Nao baadhi ya washiriki wa mdahalo huo wakiwemo wanafunzi, wamesema wamepata uelewa mpana kuhusu madhara ya ukatili dhidi ya watoto, na wameahidi kuwa sehemu ya kupinga vitendo hivyo.