Highlands FM
Highlands FM
1 June 2025, 20:46

Kadri Uchaguzi Mkuu wa Oktoba unavyokaribia, wito umetolewa kwa Watanzania kulitanguliza taifa katika maombi
Na Samwel Mpogole
Wakati Taifa likielekea kwenye Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba mwaka huu, wananchi wamekumbushwa umuhimu wa kulitanguliza taifa katika maombi, huku viongozi wanaotarajiwa kuwania nafasi mbalimbali wakihimizwa kuwa waadilifu na kuweka mbele maslahi ya umma pia kuepuka siasa za kuchonganisha wananchi.
Wito huo umetolewa katika ibada maalum iliyofanyika katika makao makuu ya Kanisa la Kinjilisti la Moraviani Tanzania, Ipyana – wilayani Kyela, ambapo ASKOFU Mchungaji Joseph Katakelu mwambungu wakanisalakiinjilist la Moravian Tanzani aliwasilisha ujumbe mzito wa kutafakari hali ya taifa na kuombea uchaguzi wa amani.
Katika ibada hiyo, mgeni rasmi alikuwa Zakayo Chang’a, Mkuu wa idara ya uhasibu Wilaya ya Kyela, aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya hiyo, Bi. Josephine Manase. Chang’a alitumia fursa hiyo kuwasilisha salamu za serikali na kuwataka wananchi kuendelea kuiombea nchi hata baada ya uchaguzi.
Nao baadhi ya waumini wa kanisa hilo wamesema ujumbe wa ibada hiyo umewagusa, wakisisitiza umuhimu wa kila Mtanzania kushiriki uchaguzi kwa amani, kuheshimu tofauti za kimtazamo na kulinda mshikamano wa kitaifa.
Ibada hiyo imeonesha dhamira ya kanisa kushiriki katika ujenzi wa taifa lenye maadili, mshikamano, na moyo wa maombi, hasa katika kipindi hiki nyeti cha kuelekea uchaguzi mkuu.