Mkoani FM

Pemba kuhifadhi mikoko kwa vizazi vya baadaye

27 July 2025, 10:56 am

Afisa Mdhamini Wizara ya Kilimo, Maliasili na Mifugo Pemba Injinia Idrisa Hassan Abdalla akipanda miti ya mikoko pamoja na wananchi. (Picha na Amina Massoud)

Shehia ya Shidi iliyopo wilaya ya Mkoani Pemba imefanikiwa kurejesha uoto asili wa fukwe za bahari kwa kupanda miti aina ya mikoko 2,500.

NA AMINA MASSOUD JABIR 

Wanannchi wa shehia ya Shidi Wilaya ya Mkoani Pemba wametakiwa kujitathmini na kujilinda kwa kuendelea kupanda  miti ya mikoko katika fukwe zao, ili kuepukana na athari zinazoweza kujitokeza  pamoja na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Kauli hiyo ametolewa na Afisa Mdhamini Wizara ya Kilimo, Maliasili na Mifugo Pemba Injinia Idrisa Hassan Abdalla mara baada ya kupanda miti ya mikoko pamoja na wananchi ikiwa ni katika kuadhimisha Siku ya Mikoko Duniani.

Amesema, kuna haja ya jamii kubadilika kwa kupanda na kuitunza miti hiyo kwani ina faida nyingi kwao ikiwemo, kupunguza maji ya chumvi kuingia kwenye mashamba, pamoja na kuwekeza kiuchumi kwa kufuga samaki, kutengeneza chumvi pamoja na kuhifadhi mazingira.

Sauti ya afisa Mdhamini Wizara ya Kilimo, Maliasili na Mifugo Pemba Injinia Idrisa Hassan Abdalla

Akitoa taarifa ya kitaalam Afisa Mkuu Idara ya Misitu Pemba Samira Makame Juma amesema, serikali imeamua kuchagua shehia hiyo kutokana na fukwe yake  iliathirika sana kwa kukatwa miti, ingawa kwa sasa wameanza kuirejesha katika uasili wake kwa kupanda miti ya mikoko 2,500, hivyo aliwataka wananchi waendelea kupanda miti ili kuepusha mmong’onyoko wa fukwe.

 Suti ya afisa Mkuu Idara ya Misitu Pemba Samira Makame Juma

Kwa upande wake Afisa Suluhisho kutoka Shirika la Uhifadhi wa Mazingira (IUCN) Suleiman Massoud Mohamed amesema, wanatekeleza miradi tofauti kwa lengo la kuwawezesha wananchi kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kurejesha asili yake, kwani mikoko ina faida nyingi kwa mazingira na kwa wanajamii.

Naye Afisa Jinsia kutoka Reasea Grace Thomas amewataka wanaume kuwashajihisha wanawake katika kuchangamkia fursa zilizomo katika kamati za uvuvi za shehia kwani maendeleo yakipatikana hayaji kwa wanawake pekee bali hata kwa jamii yote.

Suti ya afisa jinsia kutoka Reasea Grace Thomas

Akisoma risala ya Kamati ya Uvuvi shehia hiyo, Salha Saleh Riyas amesema, kazi yao ni kulinda eneo la bahari kuhakikisha linakuwa na tija kwao na kwa taifa, kwa kupanda mikoko, kurejesha viumbe vya baharini vilivyotoweka, kuotesha miche na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Picha ya wanchi walioudhuria katika maadhimisho ya siku ya Mikoko Duniani yalifanyika katika shehia ya Shidi Mkoani Pemba (Picha na Amina Massoud)

Kwa upande wake Mwananchi Rajab Abdalla Tabin amesema kuwa, kupitia miti hiyo wanatarajia faida kubwa kwani maji hayatoingingia tena kwenye mashamba yao ya mpunga na eneo hilo litarudi katika uhalisia wake wa zamani.

Akitoa ushuhuda Mwananchi Samira Seif Amesema kupitia upandaji wa mikoko kunafaida nyingi amezipata ikiwemo Kwenda nje ya kisiwa cha pemba kujifunza zaid hivyo amewataka wanawake wengine kutokubaki nyuma na badala yake wachangamkie fursa zilizopo.

Sauti ya Samira Seif

Maadhimisho ya siku ya Mikoko Duniani huadhimishwa kila ifikapo Julai 26 ya kila mwaka, kwa  mwaka huu yameadhimishwa katika shehia ya shidi Wilaya ya Mkoani Kusini Pemba ikiwa na kauli mbiu ‘KUHIFADHI MAENEO OEVU YA MIKOKO KWA VIZAZI VIJAVYO.