Mkoani FM

Wanawake someni sayansi mkaongoze meli Pemba

27 September 2023, 11:15 pm

Raya Khalfani ,Msemaji kutoka katika taasisi ya wanawake katika Sekta ya Usafiri Majini.(Picha Fatma Rashid)

Kutokana kwa uwepo wa wanawake wachache kwenye sekta ya bahari hasa kuwa mabaharia ndio asasi mbali mbali kuungana kuhamasisha maskuli ili wasome masomo ya sayansi wawepo kwenye sekta hiyo.

Na Fatma Rashid

Wanafunzi kisiwani Pemba wametakiwa kizingatia masomo ya sayansi Ili kuweza kujiunga na chuo kinachotoa mafunzo ya ubaharia.

Wito huo umetolewa na Mkufunzi wa chuo cha ubahari cha Daresalam profesa Haruna Aliy wakati akizungumza na wanafunzi wa skuli ya Mkanyageni, Mohamed Juma Pindua pamoja na Chokocho Sekondari, katika ziara ya kutembelea Skuli hizo amesema ni muhimu Kwa wanafunzi kusoma masomo ya sayansi na kujiwekea malengo mazuri ya baadae.

Amesema lengo la ziara hiyo ni kuwahamasisha wanafunzi hususani wanawake kuweza kujiunga na chuo hicho ili waweze kuwa wataalamu wazuri waliobobea katika fani za ubaharia , uinjinia urubani na nyenginezo zinnazotolewa katika chuo hicho.

Kwa upande wake Mtendaji msaidizi wa taasisi inayotoa mikopo kwa wanafunzi wanasoma masomo ya baharini (Metfund) Aloyoe S Mpazi ,amesema wanawafadhili wanafunzi wanaosoma kozi wanazozitoa na zinazohusiana na sekta ya bahari ili kuwasaidia wanafunzi waliopata ufaulu wa juu katika masomo yao na kutaka kujiunga na kozi hizo.

Nae Raya Khalfani ,Msemaji kutoka katika taasisi ya wanawake katika Sekta ya Usafiri Majini, amesema kuwa taasisi yao imeandaliwa na Shirika la Usimamizi wa Bahari Duniani kwa lengo la kuwahamasisha wanawake kujiunga na ufanyaji kazi katika sekta ya bahari.

Pia amesema tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo wapo wanawake wengi waliojiunga na kufanya kazi katika sekta hiyo wakiwemo mabaharia na waongoza meli .Kwa upande wao walimu wa Skuli hizo tatu za wilaya ya mkoani wamewashukuru watendaji wa ziara hiyo kwa kuweza kuwapa uelewa wanafunzi wao juu ya masomo yanayotolewa na chuo hicho na kusema kuwa wanatumaini kuwa wanafunzi watayafanyia kazi maelekezo yote waliyowapa.

Ziara hiyo ni moja kati ya shamra shamra ya maadhimisho ya siku ya bahari duniani ambapo kilele chake hifanyika Kila September 28 na mwaka huu yatafanyika katika viwanja vya GOmbani Pemba na kauli mbiu ya mwaka huu ni “Miaka 50 ya Marpol,Uwajibikaji wetu unaendelea”