Mkoani FM

Ukosefu wa eneo maalum la kuchomea taka baadhi ya vituo vya afya  kuathiri wananchi Pemba

14 December 2023, 6:04 pm

Eneo ambao linatumika kuchomea taka(Picha Khadija Ali)

Vituo vya afya viingi kisiwani Pemba havina maeneo maalumu ya kuchomea taka ambazp zinatokana baada ya m,abaki wanayotumia baada ya kutoa huduma kwa wagonjwa na wananchi kuwa na ghofu kupata maradhi wanaishi karibu na vituo hivyo.

Na Khadija Ali

SERA ya Wizara ya Afya ya 1990, imesema itahakikisha inaimarisha miundo mbinu mbali mbali Hospitalini ikiwemo Dawa, Usafiri, Mashimo ya kuekea Taka, pamoja na huduma za Mama na mtoto, ili kuondosha usumbufu kwa wananchi wake.

Lakini licha ya hilo bado kuna baadhi ya vituo vya Afya, vimekuwa vikilalamikiwa kutokana na kukosa miundombinu rafiki hususan, Mashimo ya kuchomea taka na kupelekea athari kwa wafanya kazi wa vituo hivyo pamoja na wananchi wanaoishi karibu na maeneo ya vituo hivyo vya Afya.

Kukosekana kwa matanuri maalum ya kuchomea taka kwa baadhi ya hospitali Kisiwani Pemba kunasababisha kuathiri afya za wananchi waliopo karibu na hospitali hizo.

Hayo yamejiri baada ya mwandishi wa habari hizi, kutembelea baadhi ya vituo sita  kisiwa Pemba, ikiwa ni pamoja na kituo cha Afya Bagamoyo, Wesha, Pujini,Vikunguni, Mgelema na Mbuzini na kubaini changamoto  ya vituo hivyo kukosa sehemu maalumu ya kuchomea taka na kupelekea kero kwa wananchi wanaoishi karibu na vituo hivyo,  jambo ambalo si salama kwa afya zao.

Nassra Ali Makame mkaazi wa Bagamoyo alisema kukosekana kwa shimo, malumu la kuchomea taka kunapelekea moshi kusambaa kwenye makaazi yao na kusababisha kukohoa na kupata muasho katika miili yao.

Said Bakari Makame kutoka Mbuzini alisema wanahofu watoto wao kupata maradhi, kwani wamekuwa  wakiokota  vifaa viliyokwisha tumika kama vile Sindano, Glavu,pamoja na vifaa vya kupimia ujauzito, kwa ajili ya kuchezea.

‘’Taka zinatupwa tu ovyo ovyo, watoto wetu wanaokota na kwenda kuchezea, na wengine wanatia mdomoni kabisa,’’amefahamisha.

Faidh Khamis Darusi kutoka Wesha alisema ni vyema Wizara ya Afya, kuchukua jitihada za makusudi kuboresha miundombinu ya kuhifadhia taka vituo vya afya, ili kulinda usalama wa afya kwa watoto.

‘’Ipo haja kwa Serikali kufanya maboresho ya kuweka eneo malumu kwa ajili ya kuchomea taka, bila ya kuleta athari kwa wananchi,’’ameeleza.

Akitaja changomoto inayowakwaza katika Hospitali yao Mkuu wa kituo cha Afya Bwagamoyo Asha Juma Khamis, alieleza ni kukosekana kwa eneo malumu la kuchomea taka licha ya kupeleka taarifa sehemu husika lakini bado changamoto hiyo haijatatulika.

Mkuu kituo cha Afya Pujini Nassra Abdallah Juma na Mkuu wa kituo cha afya Mbuzini Fatma Habib Ali walisema wanalazimika kuchoma  taka hizo kwenye mashimo ya kawaida hali inayowaathiri wakaazi wa maeneo karibu na vituo hivyo.

Mkuu kituo cha afya Vikunguni Rahma Yussuf Mohamed  na Mkuu kituo cha afya Mgelema wameishauri serikali kuwakea mashimo maalum kwa ajili ya kuchomea taka hizo kwani waathirika wakubwa ni wananchi na hasa watoto ambao wanacheza karibu na maeneo ya vituo hivyo

Hali ilivyo sasa kwa vituo tajwa hapo juu wanatupa taka katika mashimo ya kawaida, hali inavyotakiwa kwa mujibu wa miongozo ya Wizara ya Afya kwa vituo vya afya taka zinatakiwa zihifadhiwe kwenye mashimo maalum au kuhifadhiwa katika viboksi maalum vilivyopo katika vituo vya afya kwa zile taka ambazo si salama.

Katika kutafuta ufumbuzi suala hili, Mwandishi wa makala hii amezungumza na Afisa Mdhamini Wizara ya Afya Khamis Bilali Ali, amekiri kuwepo kwa tatizo  alisema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na shirika la kuhudumia watoto duniani [UNICEF] wapo katika mikakati ya kuanza ujenzi wa tanuri katika eneo la Kwareni Vitongoji, kwa ajili ya kuchomea taka kutoka Hospitali zote za Pemba, ili kuepusha uchafuzi wa mazingira ambao unasababishwa na uchomaji wa taka kiholela.

Ambapo jumla ya Sh  billion 2.5 imetengwa kwa ujenzi huo wa matanuri kwa Unguja na Pemba.