Mkoani FM

Idara ya Tiba Pemba: Endeleeni kutumia vyandarua kumaliza ugonjwa wa malaria

9 September 2023, 1:37 pm

Ugonjwa wa malaria bado upo visiwani Zanziabr hivyo jamii inatakiwa kutumia vyandarua vinavyotolewa na serikali kupitia Wizara ya Afya kitengo cha malaria kwa kushirikiana na  wahisani  mbalimbali wa maendeleo  kwa ajili ya kujifunika na sio kuvifunga kwenye bustani za bogaboga  katika maeneo yao.

Mkuu wa Idara ya Tiba Wizara ya Afya Pemba Massoud Suleiman Abdallah, wakati akizungumza na waandishi wa habari kisiwani Pemba.(Picha Khatib Nahoda)

Habiba Zarali, Pemba

MKUU wa Idara ya Tiba wizara ya Afya Pemba Massoud Suleiman Abdallah, amewataka wananchi kisiwani humo, kuvitumia vyandarua kwa ajili ya kujikinga na maambukizi ya malaria, na sio kwa kuhifadhi vipando, kama baadhi yao wanavyaofanya.

Kauli hiyo aliitowa wakati akizungumza na waandishi wa habari, juu ya hali halisi ya ugonjwa wa malaria na  mikakati ya kumaliza kabisa maradhi hayo.

Amesema lengo la kutolewa vyandaruwa ni kujifunika ili wasipate maambukizi na sio kuvitumia kwa kuzungushia vipando vyao, kama wanavofanya baadhi ya wananchi.

Ameeleza wizara kupitia kitengo cha kupambana na malaria, hutowa elimu na kuhamasisha utumiaji wa vyandarua lakini bado jamii, inaonekana kudharau elimu hiyo.

Mkuu wa Idara ya kinga Wizara ya Afya Pemba Massoud Suleiman Abdallah.

Akitowa takwimu za ugojwa huo kisiwani Pemba, ofisa uchunguzi kitengo cha malaria Pemba, Bimkubwa Khamis Kombo amesema, kesi zimepungua kutoka 471 kwa mwaka 2022, na kufikia 232 kwa mwaka huu.

Akizungumzia kwa wilaya ameeleza Chakechake alisema inaongoza kesi kutoka nje ya Zanzibar na kufikia 56, huku kesi kutoka ndani zikiwa 12.

Wilaya ya Micheweni inaongoza kwa kesi za ndani kwa kufikia 40 na za nje 24, wakati wilaya ya Mkoani kesi za nje ni 17 na za ndani 20, wakati Wilaya ya Wete kesi za nje 46 na za ndani zimefikia 17.

Ofisa uchunguzi kitengo cha malaria Pemba, Bimkubwa Khamis Kombo.

Mapema Mratibu kitengo cha malaria Pemba Makame Mohamed Kombo, amesema kwa sasa malaria iko chini ya asilimia moja na lengo ni kumaliza ifikapo 2026.

Akiitaja mikakati ya kumaliza malaria amefafanua ni pamoja na kutowa elimu, kupiga dawa majumbani pamoja na kutowa vyandarua bure kupitia kwenye shehia na vituo vya afya.

Hivyo aliitaka jamii kutokula dawa bila ya kufanyiwa uchunguzi na wataalamu wa afya kwani ni hatari kwa maisha yao.

                              MWISHO.