Mkoani FM

Serikali kuwapa wakulima mbinu mpya za kilimo Zanzibar

10 October 2023, 11:03 pm

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mh. Othamn Masoud Othmani (Picha Said Omar)

Wakulima Zanzibar wametakiwa kulima kilimo cha kisasa ili waendane na mapinduzi makubwa ya kilimo ulimwenguni ili waweze kujikomboa kupitia kilimo kwa kujihakikishia kupata chakula cha uhakika.

Na Fatma Rashid

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mh. Othamn Masoud Othmani amesema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imewaingiza wakulima katika teknolojia ya uzalishaji na utumiaji wa maji wenye tija kwa mazao ya chakula ili wakulima waondokane na kilimo cha mazoea.

Mh. Othman amesema serikali imewaingiza wakulima katika teknolojia ya kilimo cha umwagiliaji maji kwa matone kwa takribani asilimia 20.

Ameyasema hayo katika uzinduzi wa siku ya chakula duniani yaliyofanyika Chamanangwe mkoa wa Kaskazini Pemba. Amesema lengo la teknolojia hiyo ni kuhakikisha uzalishaji wa maji na utumiaji wa maji wenye tija kwa mazao ya chakula na kuondokana na kilimo cha mazoea na kuelekea katika kilimo cha biashara.

Aidha amesema lengo la maadhimisho hayo ni kuhimiza mapinduzi katika sekta ya kilimo kwa kuelimisha mbinu bora za kilimo, ufugaji na uhifadhi wa misitu na mazao yake.

Kwa upande wake Waziri wa Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar Shamatta Shaame Khamis amesema maadhimisho hayo yamewakutanisha wakulima na wajasiriamali kwa takribani miaka minne sasa tangia kufanyika Pemba kwa lengo la kujibiwa maswali yao na kutatuliwa changamoto zao.

Naye Mkuu Wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatib amesema lengo kubwa ni kuwa na mbegu moja katika sehemu moja kwa lengo la kulitambulisha zao na sehemu linapozalishwa .

Pia amesema kuwa kupitia fursa hiyo wananchi wameonesha mabadiliko makubwa katika maeneo yao kutokana na kuyafanyia kazi yale yote waliyojifunza .

Maadhimisho ya siku ya chakula duniani hufanyika Oktoba 10 ya kila mwaka ambapo kwa mwaka huu yamefanyika Chamanangwe mkoa wa Kaskazini Pemba na yataendelea hadi kufikia kilele chake tarehe 16 mwezi huu na kauli mbiu ya mwaka huu ni maji ni uhai, maji ni chakula.