Mkoani FM

ZEC kutoa  tarehe ya uchaguzi mdogo Mtambwe

14 September 2023, 4:53 pm

Mwenyekiti wa Tume ya uchaguzi Zanzibar Jaji George Joseph(Picha na Khadija Ali)

Kufuatia kifo cha aliyekuwa  Mwakilishi wa jimbo la mtambwe Habibu Ali Mohamed, tume ya uchaguzi  Zanzibar imeamua kufanya uchaguzi mdogo kuziba nafasi hiyo iliopo wazi na wadau wote wa uchaguzi wanatakiwa kushiriki kukamilisha uchaguzi huo kama ilivyokusudiwa.

TUME ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imewaomba wananchi, wapiga kura wa jimbo la Mtambwe, vyama vya siasa, wenye nia ya kugombea, na wadau wengine wa uchaguzi kujitayarisha na kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mdogo unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28 mwaka huu.

Akifungua Mkutano wa siku moja katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Wete Pemba, Mwenyekiti wa Tume ya uchaguzi Zanzibar Jaji George Joseph kufuatia kifo cha aliekua Mwakilishi wa Jimbo hilo Habibu Ali Mohamed kilichotokea Machi 3 mwaka huu., amesema , kifungu cha 40 (2) (3) cha sheria ya uchaguzi namba nne ya mwaka 2018 kinajukumu la kuendesha uchaguzi mdogo si chini ya miezi minne na si zaidi ya miezi 12.

Mwenyekiti wa Tume ya uchaguzi Zanzibar Jaji George Joseph

Akitoa maelezo ya uchaguzi huo Mkurugenzi wa uchaguzi Thabit Idarous Faina amesema, tume kupitia msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo imekamilisha utaratibu wa ununuzi wa vifaa vya kupigia kura, uchapishaji wa fomu, uwajiri wa watendaji wa vituo, uteuzi wa wagombea, elimu ya wapiga kura na uwendelezaji wa daftari la kudumu la wapiga kura.

Hata hivyo, amewataka wananchi wa jimbo hilo kuhakikisha wanakwenda katika vituo vya kupiga kura wakiwa na vitambulisho vyao vya kupigia kura na kwa ambao wamepoteza vitambulisho vyao wafike katika ofisi za Wilaya kabla ya siku tatu ya uchaguzi.

Mkurugenzi wa uchaguzi Thabit Idarous Faina

Akitoa maelezo ya sheria katika uchaguzi mdogo wa jimbo hilo Mkuu wa Kurugenzi ya huduma ya sheria Maulid Ame Mohamed, amesema miongoni mwa mambo yanayokatazwa na sheria katika uchaguzi ni kujiandikisha zaidi ya mara moja, kutoa taarifa za uongo ili ateuliwe kuwa mgombea na kupiga kampeni za kibaguzi zinazohatarisha amani na usalama wa nchi.

Wakichangia mada miongoni mwa wadau wa mkutano huo Hidaya Mjaka Ali kutoka jumuiya ya watu wenye ulemavu (JUWAUZA) ameiomba (ZEC) kuangalia miondombinu rafiki kwa watu wenye ulemavu pamoja na kuwaekea wakalimani watakaowasaidia katika zoezi hilo.

Nae Asha Mohamed Ali kutoka chama cha UNDP Mkoa wa Kusini Pemba amesema, wanawake wamekua wakishiriki kugombania nafasi mbali mbali za uongozi lakini wamekua wakikata tamaa na kurejeshwa nyuma kwa kutokuwepo kwa usawa wa kijinsia.

Kwa upande wake Khamis Juma Abdalla kutoka chama cha wananchi (CUF) ameiomba (ZEC) kuandaa utaratibu mzuri katika uchaguzi huo bila ya ubaguzi ili kuondosha migogoro baina ya vyama pizani vya siasa baada ya kumalizika kwa uchaguzi huo.

Uchaguzi mdogo wa jimbo la Mtambwe wadi ya Welezo Oktoba 1 hadi 7 kutakua na zoezi la uchukuaji na urejeshaji wa fomu za uteuzi, Oktoba 8 itakua siku ya uteuzi, 11 hadi 26 kutakua na kampeni za uchaguzi, Oktoba 28 kutakua na upigaji kura na utangazaji wa matokeo.