Mkoani FM

Waziri Mbarawa atoa neno maadhimisho siku ya usafiri baharini

26 September 2023, 7:38 am

Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa (Picha Maktaba)

Usafiri wa baharini ni usafiri salama kama vile maeneo mengine yanayotoa huduma za usafiri hivyo wananchi tutumie usafiri wa baharini kwa shuguli zetu mbalimbali za kimaisha kwani ni sehemu salama na Tanziania imeimarisha utoaji wa huduma za usafiri baharini

Na Fatma Rashid.

Waziri wa Uchukuzi Tanzania Prof. Makame Mnyaa Mbarawa amewashukuru wakazi wa kisiwa cha Pemba kwa kukubali kuwa wenyeji katika maadhimisho ya wiki ya usafiri wa bahari.

Pia amesema kuwa lengo na madhumuni ya maadhimisho hayo ni kudumisha, kuimarisha, kuenzi na kukumbushana juu ya umuhimu wa usafiri wa baharini ulio salama na unaozingatia utunzaji wa mazingira kwa maendeleo ya nchi.

 

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Mawasiliano Khadija Khamis Rajab amesema kuwa mafanikio makubwa yanayopatikana yanatokana na ushirikiano mzuri  uliopo baina ya serikali mbili ya Zanzibar na Tanzania Bara pamoja na taasisi zingine.

Naye mkuu wa chuo cha bahari Dar es Salaam (DMI) Dr. Tumaini Shabani Ngurumo amesema kuwa asilimia 80 ya mizigo inasafirishwa kwa njia ya bahari na amewataka wanafunzi waliohudhuria katika maadhimisho hayo kuweza kuangalia fursa na ajira zinazopatikana katika usafiri wa baharini na kuweza kuzitumia kwani chuo kina lengo la kuanzisha mafunzo ya ubaharia kisiwa Pemba.

Hata hivyo Mwemyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar ZMA, Meja Jenerali mstaafu Said Shaaban Omari amewataka mabaharia waendeleee kujifunza ili kuendana na teknolojia na waweze kuvitumia vyombo vyote vinavyotengenezwa kwa teknolojia ya kisasa pia amewataka waweze kuwa waadilifu kazini kwani ubaharia sio uhuni.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba , Mkuu wa wilaya ya Chake Chake Abdalla Rashid Ali ametoa wito kwa wananchi wote  kutunza na kulinda mazingira ya bahari  na kutoa taarifa endapo watawaona wageni wakiingia nchini kwa njia zisizo rasmi.

Maadhimisho hayo yanafanyika duniani kote na kitaifa yanafanyika katika viwanja vya Gombani Chake Chake Pemba na kufikia kilele chake tarehe 28 mwazi huu.