Mkoani FM

Ukosefu wa maji kuwanyima wanawake usingizi kijiji cha Mjini Kiuyu

22 August 2023, 12:15 pm

Vyombo vya kuchotea maji vikiwa kwenye foleni kusubiri maji yatolewe katika kijiji cha Mjini Kiuyu.(Picha na Fatma Hamad)

Upatikanaji wa maji bado ni changamoto kubwa katika maeneo mengi Pemba hasa vijijini, jambo ambaolo linawakosesha wananchi kushiriki katika shughuli za maendeleo kikamilifu. 

Na Fatma Hamad.

Ukosefu wa huduma za maji safi na salama  bado ni kilio kikubwa kwa wananchi wa kijiji cha  Mjini Kiuyu wilaya ya Wete mkoa wa Kaskazi Pemba.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi huko kijijini kwao, Bikame Bakar Darusi,  amesema  huu  ni  mwaka wa tano  sasa  wamekuwa  wakikosa  huduma  hiyo  ya  maji safi  na salama  na kushindwa kupata maji ya kutosha ya kufanyia  shughuli zao za nyumbani.

Bakar Hamad ikiwa ni moja ya mwanakijiji amesema suala la maji limekuwa ni tatizo sugu ambalo linawatesa wanawake wa kijijini  hapo na pia hutoka kwa baadhi ya mabomba  wakati wa majira ya  saa tano  hadi tisa za usiku,  hali ambayo inapelekea wanawake kukesha kwenye foleni ya maji.

Fatma Ali na Asha Juma wanafunzi wa darasa la tano wamesema hali hiyo inawapelekea kukosa vipindi vya mwanzo vya masomo darasani  kutokana na kuchelewa kwenye kutafuta maji  kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.

 Afisa uhusiano wa Mamlaka ya Maji [Zawa]  Pemba Suleiman Anas  Masoud,  amekiri kuwepo kwa tatizo hilo kijijini hapo.

Amesema tatizo hilo linasababishwa  na kukosekana kwa matangi ya kuhifadhia maji pamoja na uchakavu wa miundombinu ya kusambazia maji.

Masoud amewataka wananchi hao kuwa na subra, kwani tayari wameshaingizwa kwenye mradi mpya ambao unamaliziwa kufanyiwa  upembuzi yakinifu, unaofadhiliwa na benk ya watu wa Ujerumani,  ambao utajenga matangi kwenye vijiji vilivyo na shida ya maji.