Mkoani FM

Uhaba wa vifaa vya kupimia VVU Unaathiri Vijana Kutambua Afya Zao Zanzibar.

4 September 2023, 9:53 am

Maafisa kutoka Wizara ya Afya Zanzibar Kulia ni Daktar Mwanraha Ali Hassan na kushoto ni Daktar Fatma Amour Yussuf wa kituo cha Uzazi mama na mtoto Mwera . (Picha TAMWA ZNZ)

Zoezi la upimaji ya vizusi vya UKIMWI Zanzibar limeshuka kila siku kutokana na uhaba wa vifaa vya upimaji katika vituo vya serikali .

Na Mwandishi wetu.

KUMEKUWA na uhaba wa kifaa cha uchunguzi wa Virusi Vya UKIMWI (HIV Kits) katika vituo vya afya vya serikali Zanzibar jambo ambalo limepelekea huduma ya upimaji wa Virusi Vya UKIMWI kusita.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika ziara iliyofanywa na Chama cha waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA-ZNZ) watoa huduma za Afya katika vituo mbalimbali vya Wilaya ya Magharibi “B” na Wilaya ya Kati Unguja, wamesema waathirika wakubwa wa uhaba huo ni Vijana,  ambao katika siku za hivi karibuni wameonesha mwamko mkubwa wa kutaka kupima VVU na kujua Afya zao hasa kupitia vituo vya huduma rafiki kwa vijana.

Wataalamu hao kutoka kituo cha  afya Fuoni, Tunguu, SUZA, Mwera, Magirisi  wameeleza wananchi hasa vijana wamehamasika kupima VVU na hufika kwa wingi kupata huduma hiyo lakini kutokana na uhaba wa kifaa hicho huduma hiyo haipatikani kwa sasa.

Sultani Shela daktari kiongozi wa kituo cha afya Fuoni, amesema tatizo hilo ni zaidi ya miezi miwili sasa vifaa havipatikani katika vituo vya huduma rafiki kwa vijana pamoja na vituo vya afya hali ambayo wateja hulazimika kwenda katika hospitali binafsi ambapo huduma hiyo hutolewa kwa malipo.

Waziri wa Afya Zanzibar Mh: Nassor Ahmed Mazrui, amekiri uwepo wa uhaba wa vifaa hivyo ambapo amebainisha kuwa tatizo hilo limetokana na kuchelewa kufika kontena lenye vifaa hivyo ambavyo hutoka nje ya nchi.

Aidha waziri huyo amewataka wananchi kuendelea kuvitumia vituo vya afya na vituo vya huduma rafiki kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali za kiafya ikiwemo uchunguzi wa VVU ambapo maambukizi yake kwa sasa yapo katika makundi maalum ikiwemo vijana wanaotumia dawa za kulevya na wanaofanya biashara ya ngono.

Ziara hiyo ya waandishi wa habari imeandaliwa na Chama cha waandishi wa habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA-ZNZ) kupitia mradi wa kuendeleza utetezi wa afya ya uzazi kwa wanawake na wasichana mijini na vijijini ambao unaendeshwa na chama hicho Zanzibar katika Wilaya mbili za Unguja ambazo ni Wilaya ya Kati na Magharibi “B” na wilaya ya Chakechake kwa Pemba kwa ufadhili wa Wellspring Philanthropic Fund (WPF) kutoka nchini  Marekani.