Mkoani FM

70% ya wakulima hulima kilimo cha mazoea Pemba-Utafiti

17 September 2023, 4:47 pm

Mtaalam wa Kilimo na Biashara Judith Paulia Senga(Picha na Khadija Yussuf)

Imeelezwa kuwa wakulima kisiwani Pemba bado wanalima kilimo cha mazoea ambacho hawazingatii  maelekezo ya kitaalam juu ya kilimo jambo ambalo linapelekea kukosa mavuno mazuri hasa wale wanaolima kibiashara.

Na Khadija Yussuf

Wakulima kisiwani Pemba wametakiwa kuacha tabia ya kulima kimazoea ili kuzalisha mazao yenye ubora na kupata soko la uhakika.

Imeelezwa  kupitia utafiti wa uendelezaji wa mbogamboga na viungo umeonesha asilimia 70 ya wakulima wanalima kilimo cha mazoea jambo ambalo husababisha kutozalisha mazao yenye ubora.

Akizungumza na wakulima, wafanyabiashara na wadau wa kilimo katika ukumbi wa Samail Gombani Chake Chake Pemba mtafiti na mtaalam wa kilimo na biashara Judith Paulia Senga amesema mradi wa Uharakishahji wa Uendelezaji wa Teknolojia una lengo la kuwajengea uwezo wakulima kuwa na mahusiano mazuri na wafanyabiashara na wataalam wa kilimo ili kuondokana na kilimo cha mazoea na kuzalisha bidhaa zenye ubora kwa lengo la kupata soko la uhakika.

Amesema utafiti huo umegundua wakulima hawana ubunifu wa kulima mazao yao kwani hulima mazao ya aina moja hali inayopelekea kuuza kwa bei ndogo, hivyo amewataka kuwashirikisha wafanyabishara na wataalam wa kilimo kujua aina ya mazao ya kupanda ili kuepusha kuharibika sambamba na kutatua changamoto za kifedha, soko, elimu na pembejeo.

Mtaalam wa Kilimo na Biashara Judith Paulia Senga(Picha na Khadija Yussuf)

Wakielezea changamoto zinazowakabili wajasirimali Said Yussu Ali wa kikundi cha Juhudi Zetu na Khadija Khamis Salum wa kikundi cha Tujikomboe wamesema ni ukosefu wa elimu ya usindikaji wa mazao na kutojua afya ya udongo na uhaba wa mbolea.

Naye Rahma Mbarouk wa kikundi cha Marwa Product kutoka Wawi wameomba kuanzishwa kwa vituo vya kulelewa wajasiriamali ili waondokane na changamoto zinazowakabili.

Bwana shamba kutoka wilaya ya Chake Chake Rashid Mohd amesema wakulima hukosa mbinu bora za upandaji wa mbegu kwa  kuweka kiwango kikubwa cha mbolea sababu inayopelekea kushindwa kuzalisha mazao yenye ubora unaotakiwa, hivyo amewashauri kuwashirikisha mabwana shamba ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Akizungumzia upatikanaji wa mikopo kwa wajasiriamali Kaimu Mratibu Mitaji na Mikopo kutoka Ofisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji Pemba Haji Khamis Haji amesema serikali ya awamu ya nane kwa kushirikiana na Bank ya CRDB imetoa mikopo ya ahueni ya uviko19 ambapo jumla ya Tsh million 7 kwa upande wa Pemba zimetolewa kwa kundi hilo na kuwataka wajasiriamali kuanzisha vikundi kwani mkopo hautolewi kwa mtu mmoja mmoja na kuwataka bidhaa azipelekwe kwa wataalum wa viwango ili ziwe na thamani zikiwa sokoni.

Kaimu Mratibu mitaji na Mikopo kutoka Ofisi ya Rais Kazi Uchumi na Uwekezaji Pemba Haji Khamis Haji

Mradi wa Uharakishaji na Maendeleo ya Teknolojia unatekelezwa na shirika la kimataifa la utafiti na uendelezaji wa mazao na mbogamboga na viungo kwa ufadhili wa USAID, IFDC na CIMMYT ambapo jumla ya vikundi 20 vya wilaya ya Chake Chake vimefikiwa na mradi huo.