Mkoani FM

Wanamtandao Pemba waaswa kuendeleza mapambano dhidi ya udhalilishaji wa kijinsia

12 September 2023, 1:57 pm

Zaina Abdalla Salim afisa mradi wa kupinga vitendo vya udhalilishaji Tamwa Zanzibar (Amina Amasoud)

Matendo ya  udhalilishaji kisiwani Pemba bado yapo hivyo kumekuwa na mtandao maalum wa kupinga matendo hayo kwa kufuatilia kesi hizo na kutoa elimu ili kuhakikisha jamii inabaki salama.

Na Amina Masoud

Wanamtandao wa kupinga udhalilishaji wa kijinsia kisiwani Pemba wametakiwa kuendeleza juhudi za kutoa elimu na kuibua vitendo hivyo ili jamii kupata uwelewa zaidi.

Wito huo umetolewa na afisa mradi wa kupinga vitendo vya udhalilishaji kutoka Tamwa Zanzibar Zaina Abdalla Salim wakati wa uwasilishaji wa ripoti ya utekelezaji kwa kipindi cha miezi mitatu kwa wanamtandao wa kupinga ukatili na udhalilishaji wa kijinsia kisiwani Pemba uliofayika katika ukumbi wa ofisi hizi Mkanjuni wilaya ya Chake Chake Pemba.

Amesema wanamtandao wanayo nafasi kubwa katika kuibua kesi hizo kwani hapo awali wamefaya kazi nzuri jambo ambalo limewezesha jamii kupata mwamko wa kuripoti kesi hizo hivyo ni vema kuedeleza juhudi zao ili jamii iondokane na janga hilo na kulifaya kundi la wanawake na watoto waishi katika mazingira salama.

Kwa upande wake mratibu wa Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake TAMWA Pemba Fathiya Mussa Said amewataka wanamtandao hao kuelimisha jamii kuondokana na mtazamo wa kutaka kubadilishwa sharia ya mtoto kuanzi miaka 15 hadi 17 kutambulika kuwa ni mtu mzima kwani kufanya hivyo kunaweza kuleta madhara makubwa kwa watoto kwani wengi wao bado hawajaweza kujitambua.

Kwa upande wao wanamtandao wamesema imefika wakati sasa kwa wazazi walezi kufuatilia mienendo ya watoto wao kwa karibu ili iwe rahisi kubaini viashiria vya vitendo hivyo viovu na kuwataka jamii kutoa ushirikiano endapo watuhumiwa wa kesi hizo wanapopatikana kwa lengo la kumaliza matendo hayo.

Aidha wameeleza changamoto kubwa ni watuhumiwa kukimbia kabla ya kupelekwa kwenye vyombo vya sheria pamoja na kuwepo kwa kesi za watoto wanaokinzana na sheria.

Mkutao huo wa siku moja wa uwasilishaji ripoti ya utekelezaji kwa kipindi cha miezi mitatu umewakutanisha wanamtandao kutoka Wilaya ya Wete, Micheweni na Mkoani, viongozi wa dini pamoja na maafisa dawati ya jinsia.